Wednesday, January 16, 2008

Sakata la BoT - Mramba ageuka bubu!

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha wakati ukifanyika ubadhirifu wa mamilioni ya shilingi kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Basil Mramba, amekataa kuzungumza lolote kuhusu sakata hilo.

Mramba ambaye hivi sasa ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, alikataa kueleza lolote kuhusu suala hilo ambalo Jumatano ya wiki iliyopita lilisababisha aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali apoteze wadhifa wake huo.

“Tafadhili, naomba unisamehe. Sipo kwenye nafasi ya kuzungumzia suala hilo. Kama ni ile EPA ya Economic Partnership Agreement nitasema, lakini siyo hiyo,” alisema Mramba.

Wakati Mramba akipata kigugumizi kuzungumzia suala hilo, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, kwa upande wake amesema hana wasiwasi wowote kuhusu hatima yake katika suala hilo.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Waziri Meghji alieleza kushangazwa na watu wanaomhusisha na tuhuma hizo, huku wakijua kuwa hausiki nazo kwa namna yoyote.

Waziri Meghji alisema anatambua vyema kwamba, uamuzi wake wa kuwanyima baadhi ya watu misamaha ya kodi, ikiwa ni pamoja na hatua nyingine za kiudhibiti alizozichukua, ni sehemu ya mambo iliyomjengea maadui ambao sasa wanataka kuitumia kashfa ya EPA kumtaka awajibike.

“Sina wasiwasi, niko imara kwa kuwa natambua kwamba sijatenda kosa lolote katika sakata hili zima… najua kuna watu ambao wanafanya mambo haya kwa sababu tu ya maamuzi niliyochukua ya kuwanyima exemptions (misamaha ya kodi),” alisema Meghji.

Barua za Wizara ya Fedha ambazo Tanzania Daima imeziona zinaonyesha kuwa, Septemba 15 mwaka 2006, Waziri Meghji aliandika barua kwenda kwa kampuni ya ukaguzi wa kimataifa iliyokuwa ikikagua mahesabu ya BoT ya Deloitte & Touche akitetea malipo ya dola za Marekani 30,732,658.82 kwenda kampuni ya Kagoda Agriculture ambayo sasa inahusishwa na ubadhirifu kupitia kashfa hiyo ya EPA.

Katika barua hiyo, Meghji amekaririwa akisema kwamba fedha hizo zilikuwa zimetolewa kwa matumizi maalum ya siri kwa idhini ya serikali na akawataka wakaguzi hao kutambua kuwa suala hilo lilifanywa kwa kuzingatia sheria za nchi.

Hata hivyo, barua nyingine inaonyesha kuwa, siku nne baada ya kuandika barua hiyo (yaani Septemba 19, 2006), Waziri Meghji alibadili uamuzi huo na akaiandikia kampuni hiyo ya ukaguzi barua nyingine ya kufuta barua yake ya awali.

Meghji katika barua yake hiyo ya pili anakaririwa akisema kwamba, barua yake ya kwanza ilikuwa imeandaliwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali ambaye kimsingi ndiye aliyempa ushauri wa kuiandika ile ya kwanza.

Katika barua yake hiyo ya pili, Meghji aliandika kwamba, alikuwa amelazimika kuifuta barua yake ya awali baada ya kutambua kuwa, malipo hayo kwa Kagoda Agriculture hayakuwa sahihi kwa taratibu za kiserikali.

Meghji alieleza kushangazwa kwake na kuibuka kwa mjadala katika intaneti, ambao umekuwa ukimhusisha na sakata hilo la EPA ilhali ikijulikana bayana kwamba matukio yaliyobainisha kupotea kwa shilingi bilioni 133 yalitokea wakati yeye akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

“Mimi nashangazwa sana na mjadala huu unaopinduliwa hivi sasa. Watu wanaijadili kashfa hii kama vile mimi ndiye nilikuwa Waziri wa Fedha mwaka 2005 wakati hayo yakitokea,” alisema Meghji kwa uchungu.

Waziri Meghji alisema pia kwamba, yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuamuru kufanyika kwa uchunguzi katika akaunti hiyo ya EPA, Desemba 4, 2006 miezi kadhaa kabla suala hilo halijafika kabisa bungeni.

Wakati sakata hilo likiendelea, imebainika kwamba, Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyopo sasa hivi watamaliza muda wao Jumamosi ya wiki hii na hivyo kutoa fursa kwa bodi mpya kuanza kazi.

Taarifa ya BoT kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana inaeleza kwamba, bodi hiyo mpya inayoanza kazi Jumatatu ya wiki ijayo baada ya kuzinduliwa na Waziri wa Fedha, chini ya uenyekiti wa Gavana mpya, Profesa Benno Ndulu, imeshajipanga kwa ajili ya kuanza kutekeleza kazi iliyopewa na Rais Jakaya Kikwete ya kukutana na kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wa BoT walio chini ya mamlaka yake, ambao walihusika kwa namna moja au nyingine katika sakata la EPA.

Wakurugenzi wa bodi hiyo iliyoundwa Novemba 2007 ni, Profesa Ndulu ambaye ni Mwenyekiti na Gavana, Dk. Enos Bukuku, Juma Reli na Lila Mkila.

Wengine ni Profesa Haidari Amani, Ali Mufuruki, Dk. Natu Mwamba, na mwingine atakayetoka Zanzibar, ambaye bado hajateuliwa.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kutoka Jamhuri ya Muungano na Katibu Mkuu Hazina kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambao wote wanaingia kwa nyadhifa zao.

Mjumbe wa mwisho wa bodi hiyo ni Bosco Kimela, ambaye ndiye anakuwa Kaimu Katibu wa Bodi.

Taarifa hiyo ya BoT imesema kwamba, mara baada ya bodi hiyo kuzinduliwa, Gavana Ndulu ataitisha mkutano mara moja na kuanza kuyafanyia kazi maelekezo ya rais kwa bodi hiyo kufuatilia kashfa ya EPA.

Tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa BoT zilitolewa hadharani kwa mara ya kwanza na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2007/08 na baadaye akapanga kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kulichunguza suala hilo.

Katika tuhuma hizo, Dk. Slaa alinukuu taarifa kadhaa kutoka katika mtandao wa intaneti zilizokariri baadhi ya majina ya watu, akiwamo Ballali na akaorodhesha jinsi ambavyo wamekuwa wakihujumu fedha za umma kupitia BoT. Hata hivyo, kwa nyakati tofauti hoja hizo za Slaa zilionekana kutiliwa shaka na viongozi kadhaa wa juu serikalini.

Hata hivyo, siku chache baadaye, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwa nyakati tofauti walikiri kuwa serikali ilikuwa na taarifa kuhusu tuhuma katika akaunti ya EPA na wakaahidi kuwa tayari serikali ilikuwa imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuitafuta kampuni ya kimataifa ya ukaguzi kuzifanyia kazi.

Kwa upande wake, wakati kikao hicho cha bajeti kikiendelea, Lowassa, alikaririwa akisema kuwa tuhuma hizo zinashtua na kuwa serikali ilikuwa inazifanyia kazi kwa umakini.

Kana kwamba haitoshi, Septemba 15 mwaka jana, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mwembeyanga Temeke, Dar es Salaam, Dk. Slaa alitaja orodha ya majina 11 ya viongozi kadhaa wa serikali, akiwatuhumu kwa ufisadi likiwamo jina la Ballali.

Kuundwa kwa EPA kulitokana na upungufu wa fedha za kigeni serikalini kati ya miaka ya 1970 na 1990 hivyo, BoT ilipewa jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za kigeni kwa niaba ya serikali.

Kabla ya jukumu hilo kukabidhiwa rasmi BoT, kazi za EPA zilifanywa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Lakini, Juni 1998 iliamuliwa kuwa zifanywe na BoT.

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home