Monday, January 14, 2008

Utoto wa Zitto uko wapi?

KABLA ya kwenda mbali, niweke sawa jambo hili; kwamba kuna watoto wenye akili ya watu wazima na kuna watu wazima wenye akili ya kitoto.

Hii inatokea pote duniani si Tanzania tu. Unakuta watoto, vijana wana hekima na busara kuliko watu wazima, na watu wazima bado wananyonya vidole na kufungwa nepi!

Mfano mtu mzima anayehongwa milioni moja na kuachia mabilioni yakaondoka, au mtu anayeteketeza maslahi ya Taifa na kufumba macho wakati rasilimali za nchi hii zinaporwa kwa vile amehongwa vijisenti, huyo bado ananyonya kidole na kufungwa nepi! Ni mtu mzima, hata kama ana miaka 50-60, bado anakuwa na akili za kitoto!

Kama Zitto Kabwe ni mtoto basi ni kati ya watoto wenye hekima na busara kuliko watu wazima; atakuwa ni mtoto mwenye akili ya watu wazima!

Nilikuwa sijaisoma barua ambayo Zitto, amemwamndikia Spika Sitta. Niliposikia kwenye vyombo vya habari kwamba Zitto, alikuwa amechukua hatua za kitoto, nilijawa na wasiwasi. Zitto, ninayemfahamu amevuka hatua ya kunyonya kidole, si mtu wa kufungwa nepi; umri wake ni mdogo sawa, lakini ni ule wa wanamapinduzi wote duniani, umri wa bwana Yesu Kristu.

Hata Mwalimu Nyerere, wakati anapigania uhuru wa Tanganyika, alikuwa kijana mdogo. Joseph Kabila, ni kijana mdogo, lakini anaweza kuiongoza DRC pamoja na matatizo makubwa ya nchi hiyo. Ipo mifano mingi wa vijana wanaopambana kiutuuzima.

Nimepata bahati ya kusoma barua hiyo kwenye gazeti hili toleo lililopita. Nimeisoma zaidi ya mara tano, nikitafuta Utoto wa Zitto. Nimejitahidi sana kuona ni wapi kijana huyu kakosea. Maneno yake yote yamepimwa vizuri, kanuni za Bunge, amezizingatia. Kosa lake liko wapi? Kumwandikia Spika au barua ya Spika kuonekana kwenye mtandao? Vyombo vya habari vilimnukuu Spika Sitta, akiilalamikia barua ya Zitto, kwamba kwa barua hiyo Zitto hakuonyesha ukomavu wa kisiasa na ni dalili za ‘Utoto’.

Vyombo vya habari vyenye uchokozi viliiweka hivi ‘Spika Sitta amsikitikia Zitto’. Baada ya kuisoma barua ya Zitto, nimejiuliza maswali: je ni utoto wa Zitto au ni kuchoka kwa Sitta?, je ni utoto wa Zitto au ni dalili za Sitta kushindwa kusoma alama za nyakati?




SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta

Inaonekana Spika Sitta, anaelekea kuchoka na kushindwa kusoma alama za nyakati. Juzi juzi alikuwa mtu wa kwanza kupinga ripoti ya utafiti wa REDET kwamba hadhi ya Bunge imeshuka. Vyombo vya habari vilimnukuu akisema: “ Sikubaliani na matokeo ya utafiti huo. Mimi nina uzoefu wa siku nyingi katika masuala ya Bunge. Inashangaza sana wakati huu Bunge lina kanuni mpya zinazoimarisha utendaji wake, lakini utafiti unaonyesha wananchi hawana imani.

Bunge limekwisha kukamilisha kufanya mabadiliko katika kanuni zake ambazo ni tofauti na za awali. Kanuni za sasa zinalipa nguvu zaidi Bunge katika utendaji. Inashangaza sana haya matokeo. Kanuni zetu ni mpya na ni nzuri.

Inawezekana hii taasisi (REDET) iliyofanya utafiti ni chombo tu kinachojitafutia umaarufu”.

Kama si kuchoka ni nini? Spika Sitta, anasema Bunge lina kanuni mpya, na wakati huo huo anasema Barua ya Zitto ni ya kitoto na ni ya mtu ambaye hakukomaa kisiasa. Labda tatizo ni kwa vile Zitto, anasema kwamba ikibainika Bunge, lilikosea, limwombe radhi. Bunge, lenye kanuni nzuri ni lazima lifanye hivyo! Inawezekana Bunge, halikosei? Bunge linaundwa na malaika watupu? Tunajua kabisa kwamba Bunge ni chombo kitukufu, lakini linaundwa na watu, linaundwa na vyama vya kisiasa. Bunge, letu karibia ni la chama kimoja, chama ambacho kinashutumiwa kuiba kura wakati wa uchaguzi, kinashutumiwa kwa rushwa na ufisadi; wingi wa wabunge wa chama hiki ndani ya Bunge unaweza kulisukuma Bunge, kufanya makosa. Mfano mzuri ni kesi ya Zitto.

Kama Spika Sitta, asingekuwa mwanachama wa CCM, kesi ya Zitto, isingekuwa kama ilivyokwenda. Ilionekana wazi, hata kwa mtu mwenye akili ndogo kabisa, kwamba Wabunge wa CCM na wakiwa na Spika wao, walikuwa wakitetea maslahi ya chama chao, si maslahi ya Taifa.

Zitto, alikuwa akitetea maslahi ya taifa kwa kuhoji mkataba wa Buzwagi. Lakini mjadala uliofuata, ulitoa picha ya CCM kupambana na wapinzani. Hata wabunge wa CCM, tuliowazoea kuwasikia wakitetea maslahi ya Taifa, walifunga midomo yao wakati wa mjadala wa Buzwagi. Waliweka chama mbele na Taifa nyuma. Aibu!

Nafikiri hapa kuna somo. Kuna haja ya Katiba mpya. Na kuangalia namna mpya ya kumpata Spika wa Bunge. Kuna haja Spika wa Bunge, kutoka nje ya vyama vya Siasa. Tukio kama la Zitto na sasa matukio ya Kenya, yanatufundisha. Spika wa Bunge na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ni wawe ni watu wasiokuwa na upande wowote.

Wawe ni watu wanaoheshimika katika jamii, watu wasiokuwa na uchu wa mali na madaraka, watu wenye uzalendo unaozidi mipaka. Tumejifunza kwamba kumbe Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kama ameteuliwa na Rais aliye madarakani au kama ni mwanachama wa chama tawala, basi atatenda kwa maelekezo ya Rais au maelekezo ya chama chake.

Ijionyesha wazi katika Katiba, kwamba Spika wa Bunge na Mweneyekiti wa Tume ya Uchaguzi ni watu wasiofungamana na upande wowote.

Yaliyotokea Kenya, yanaweza kutokea hapa. Ubabe wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya Samuel Kivuitu wa kutangaza aliyeshindwa, kwa vile yuko madarakani, hauna tofauti na kile anachokiita Zitto ‘abuse of majority’. Adhabu yake ilitolewa ‘kiubabe’ na Bunge, kwa vile ‘majority’ ni wabunge wa CCM.

Je, kesho na keshokutwa ikijitokeza CCM kushindwa, watakubali hawa? Si watakuwa kama Mwai Kibaki? Hivyo tusimpuuze Zitto. Tumsikilize na kuhakikisha mbegu mbaya za kutuiingiza kwenye machafuko zinachambuliwa na kutupwa motoni!

Kwenye barua yake, Zitto anamwabia Spika Sitta:

“Mheshimiwa Spika, kwa misingi ya kanuni zetu nilizonukuu hapo juu ninaleta kwako maombi ili Kamati ya Kanuni za Bunge ipitie upya adhabu niliyopewa na Bunge ambayo mimi ninaamini haikuwa halali, haikufuata Kanuni za Bunge, haikuzingatia tamaduni za Bunge (maamuzi ya Bunge yaliyopita) na kubwa zaidi haikunipa nafasi ya kujitetea”.

Utoto uko wapi kwenye hoja hiyo hapo juu? Kama kanuni zilifuatwa, Spika Sitta, amjibu Zitto. Kama ni kweli Zitto, alipata nafasi ya kujitetea, Spika Sitta, aonyeshe wazi. Kama ni kweli kanuni hazikufuatwa, ieleweke. Hadhi ya Bunge, itapanda, endapo wananchi watashuhudia jinsi kila kitu bungeni, kinavyofanywa kwa ukweli na uwazi. Ujana wa mbunge, jinsia ya mbunge au chama cha mbunge kisiwe kigezo cha kumnyanyasa na kumdhalilisha.




MBUNGE Zitto Zuberi Kabwe

Zitto, anaendelea kujieleza:”Mheshmiwa Spika, mimi kama Mbunge katika Bunge lako ninaamini ya kwamba adhabu niliyopewa ilifikiwa kwa shinikizo la kiitikadi na hata kufikia kundi moja la wabunge kutumia vibaya wingi wao bungeni (abuse of majority) na kuniadhibu bila kufuata kanuni za Bunge”.

Utoto uko wapi kwenye hoja ya hapo juu. Bahati nzuri Shughuli za Bunge hutangazwa moja kwa moja. Sote tuliona ushabiki na shinikizo la kiitikadi. Haiwezekani kwamba hakuna hata mbunge mmoja wa CCM, ambaye hakuguswa na mkataba wa Buzwagi.

Haiwezekani kwamba wabunge wote wa CCM, walifurahishwa na mkataba wa Buzwagi. Inawezekana kwamba walikuwa hawajafuatilia, lakini baada ya maelezo ya Zitto, kwa nini hawakuchukua hatua ya kufuatilia?

Zitto, bado anaonekana ni mtu mwenye busara kubwa, maana kwenye barua yake anaonyesha heshima aliyonayo kwa Bunge: “ Mheshimiwa Spika, licha ya kwamba nina nafasi na haki ya kuomba chombo kingine cha dola kama Mahakama kupitia adhabu hii, nimesita kufanya hivyo ili kulipa Bunge nafasi ya kujikosoa”.

Kuna utoto kwenye maneno hayo hapo juu? Ni kweli Zitto, ni mdogo wa umri, lakini mawazo yake na matendo yake ni ya mtu mzima, tena mtu mzima mwenye hekima na busara. Hoja zake zinaonyesha uzalendo wa hali ya juu. Kumpuuza ni kujiabisha, na kwa mambo kama hayo hadhi ya Bunge itaendelea kudidimia.

Kinachojionyesha wazi kwenye barua ya Zitto, ni kwamba Spika Sitta, alishindwa kulisimamia vizuri swala lake:

“Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, wewe Mheshimiwa Spika ndiye unapaswa kuhakikisha kuwa utaratibu Bora unafuatwa bungeni..Kanuni 58(1)”.

Malalamiko ya Zitto, yanaonyesha wazi kwamba kama Spika Sitta, asingekumbwa na kirusi cha ushabiki na itikadi, adhabu iliyotolewa dhidi yake isingetolewa.

Ukweli ulio wazi, ambao inashangaza sana Spika Sitta, hauoni, ni kwamba hadhi ya Bunge, imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya adhabu ya Zitto. Wengi waliofuatilia matangazo hayo walikatishwa tamaa na uamuzi wa Bunge wa kumsimamisha Zitto.

Madini ni sekta nyeti ambayo imekuwa ikilalamikiwa. Zitto alikuwa akihoji sekta ya madini juu ya usiri wa Mkataba wa Buzwagi. Kwa vyoyote vile angekuwa na mvuto kwa Watanzania wengi wanaotilia shaka zoezi zima la uchimbaji wa madini. Hoja zake zilikuwa na ushawishi mkubwa na hadi leo hii hazijajibiwa ipasavyo.

Ingawa watu hawakufahamu Kanuni za Bunge, kwamba hoja haiwezi kutolewa juu ya hoja, kwa akili tu za kuzaliwa, waliweza kuuona uonevu aliotendewa Zitto.

Yeye analifafanua vizuri: “Mheshimiwa Spika, Bunge lina taratibu za kuleta hoja bungeni. Taratibu hizi zimefafanuliwa kinagaubaga katika Kanuni za Bunge na zimeanisha wazi kabisa ya kwamba hoja haiwezi kutolewa juu ya hoja nyingine na kwamba muda wa kutoa taarifa za hoja umewekewa taratibu ndani ya Kanuni za Bunge”.

Kwa kesi ya Zitto, hoja ya kumsimamisha ilitolewa juu ya hoja yake mwenyewe na kuamuliwa hapo hapo!

Ni bora Mheshimiwa Spika Sitta, aanze kusoma alama za nyakati. Enzi za Bunge la chama kimoja, zimepita. Enzi za mtu kuonewa, kudhalilishwa akakaa kimya zimepitwa na wakati. Enzi za kuwasikiliza wazee na kuogopa kuwakosoa zimepitwa na wakati. Enzi za chama kimoja zimepitwa na wakati. Kwa vile Taifa letu liliamua kufuata siasa ya vyama vyingi, hakuna njia nyingine zaidi ya kuwa na Bunge, linaloendana na mfumo huu mpya.

Spika Sitta, ana nafasi ya pekee kulibadilisha Bunge likawa na sura mpya. Kama anataka Tanzania, imkumbuke, basi afanye mabadiliko makubwa ndani ya Bunge letu. Juhudi zake za kutunga kanuni mpya za Bunge, ziendane na juhudi za ushawishi wa Katiba mpya ili siku zijazo Spika wa Bunge awe ni mtu asiyefungamana na chama chochote cha kisiasa.



Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa S. L. P. 114 Magu, Mwanza. Simu: 0754 633122

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home