Siasa si mchezo mchafu, kuna wanasiasa wachafu!
Na.Maggid Mjengwa
STALIN aliwahi kutamka: "Anayepiga kura hana anachoamua, anayehesabu kura ndiye anayeamua kila kitu". Tumeona uchaguzi wa Kenya ulivyokwenda. Watu wameshiriki mchakato wa kujiandikisha na hata kupiga kura bila matatizo makubwa. Kazi ikaja kwenye kuhesabu kura. Ndipo hapo hesabu zikaanza kuwa ngumu. Kukawa na kufuta hapa na pale. Kukawa na kushinikizana, na kadhalika.
Naam, kila mwenye kufikiri sasa anaelewa kuwa kiini cha vurugu za Kenya ni Tume ya Uchaguzi ambayo si Huru. Hivyo basi, dawa ya kuepuka au kupunguza shari kama inayotokea Kenya, ni kwa nchi zetu hizi kuangalia upya Katiba, na hususan, inapohusu uchaguzi na Tume ya Uchaguzi.
Vinginevyo, kinachotokea Kenya ni matokeo ya wanasiasa wachache wachafu, ambao wako tayari nchi iangamie, alimradi wao wajihakikishie wanabaki madarakani kulinda maslahi yao.
Ni wanasiasa hawa wachafu ambao wako tayari kuiba kura na hata kutumia vibaya nguvu za dola kuwakandamiza watu wao wenyewe kwa shabaha hiyo ya kubaki madarakani. Hawa ni baadhi ya viongozi katika nchi zetu ambao wamefikia kuwafanya watu waamini kuwa siasa ni mchezo mchafu. Nia ni kuwatisha raia wema wasijiingize katika siasa. Kwamba siasa ifanywe na kundi fulani la kijamii.
Si kweli kuwa siasa ni mchezo mchafu. Na tuamini kuwa kila kitu ni siasa, hata suala la wapi utatupa takataka zako ni siasa. Ustaarabu ukizingatiwa, siasa ni jambo jema na la kuvutia. Siasa ni harakati za mapambano ya hoja. Siasa ni majadiliano endelevu. Hata watu wasipokubaliana katika majadiliano ya kisiasa, basi " Hukubaliana kutokubaliana". Kamwe, siasa si mchezo mchafu, bali, kuna wanasiasa wachafu.
Kwamba siasa ni jambo jema na la kuvutia tunalishuhudia katika nchi za wenzetu zenye kuzingatia utawala wa sheria na zenye katiba zenye kulinda maslahi ya nchi zao. Kwa mfano, tunaona jinsi mchakato wa kutafuta wagombea Urais nchini Marekani unavyofanyika. Ndani ya chama kimoja watu wanashindana kwa hoja. Leo tunaona Hillary Clinton na Barrack Obama wa chama cha Democrats wakichuana kwa karibu kutafuta nafasi ya kuchaguliwa kugombea Urais kupitia chama chao. Hillary na Obama hawana chuki binafsi. Wanashindana kwa hoja. Ikifika siku mmoja wao akachaguliwa na mwingine akashindwa ustaarabu kwao ni kupongezana kwa kushikana mikono na baadaye kushirikiana katika kufanikisha ushindi wa chama chao.
Kama ni mitandao, yao huisha siku ile mshindi anapotangazwa. Hakuna kutafutana na kufanyiana hila baada ya hapo. Hiyo ndiyo maana halisi ya ushindani. Hiyo ndiyo siasa, si mchezo mchafu. Ikumbukwe, kuwa kila matokeo ya uchaguzi yana tafsiri zake. Kama ni uchaguzi huru na wa haki kuna mawili; kushinda au kushindwa. Katika hilo la mwisho, kiongozi au chama kinashindwa uchaguzi, kuna kusikitika, lakini wakati huo huo kuwapo na furaha kuona demokrasia inafanya kazi yake.
Mgombea au chama kikubali kuwa wapiga kura wamewakataa, hamkuwafanyia mengi waliotarajia, au hawaamini kuwa mtawatekelezea wanayotarajia, hivyo basi, wamewachagua wengine. Mkubali kuchukua nafasi ya wapinzani, mwangalie kasoro zenu, mjipange upya, siasa haiishii kwenye uchaguzi, kila siku ni siasa, kuna uchaguzi mwingine unakuja.
Katika nchi zetu hizi tunaona ni jinsi gani hilo la kukubali kushindwa linakuwa gumu kwa baadhi ya wanasiasa. Ukweli tu kuwa katika nchi zetu hizi Tume Huru za Uchaguzi hukataliwa na walio madarakani unathibitisha dalili za kutokuwa na utayari wa kuendesha ushindani wa kisiasa katika mazingira ya tambarare kwa pande zote zinazoshindana.
Lakini ushindani wa kisiasa mara nyingi unahusu vyama. Tatizo kuna wanaoingia katika ushindani wa kisiasa kupitia vyama na bila kujua dhana ya chama ina maana gani. Na tuanze kwa kujiuliza, je, chama cha siasa ni nini? Katika harakati za kisiasa kuna aina mbili za vyama; Chama cha Ukombozi na Chama cha Uongozi. TANU, FRELIMO, ANC ni mifano ya vyama vya ukombozi vilivyokuja kugeuka kuwa vyama vya uongozi. CCM, CUF, CHADEMA ni mifano michache ya vyama vya uongozi.
Chama imara cha ukombozi kinatakiwa kijenge uwezo wa kuwa chama cha uongozi mara ile kitapotwaa madaraka. Hufanya hivyo kwa kuweka mkazo juu ya mafunzo kwa makada wake. TANU, FRELIMO na ANC viliweza kujenga uwezo huo. Kielelezo cha nguvu na umakini wa chama cha kisiasa ni uwingi na ubora wa makada wake. Chama ni makada kwa vile chama ni itikadi, malengo na shabaha na wala si nasaba na umaarufu wa mtu mmoja mmoja ndani ya chama.
Chama chenye makada wengi wenye kuielewa itikadi, malengo na shabaha ya chama, huwa hakimtegemei mtu mmoja katika kuwapo kwake. Hakimtegemei mtu mmoja katika kufanikisha ushindi wa chama. Hakimtegemei mtu mmoja katika kuhamasisha wanachama au umma. Chama hicho hujiamini.
Edward Mondlane, kiongozi wa kwanza wa FRELIMO alipouawa kwa bomu la barua, Frelimo walijua watafanya nini, walijua mchakato gani utumike katika kumpata mrithi wake. Na hata Samora Machel, alipokufa ghafla kwa ajali ya ndege, FRELIMO walijua watafanya nini.
Na kama Nyerere angekufa wakati wa TANU, bila shaka, TANU walikuwa wamejindaa vema na wakijua cha kufanya. TANU haikuwa na ukame wa jeshi la makada. Nguvu ya FRELIMO kama ilivyokuwa kwa TANU ilikuwa ni makada wake. Na ieleweke, makada ni roho ya chama. Chama kikianza kupungukiwa na idadi ya makada wake wakereketwa, basi, chama hicho hakina mustakabali ulio salama, kitayumba na pengine kuangukia kaburini.
Tuangalie basi mfano wa chama kisichokuwa na nguvu ya makada. Wakati John Garang wa SPLM alipokufa kwa ajali ya ndege, hakuna ndani ya SPLM aliyekuwa na hakika ya nini kifanyike. Kwamba ni mke na mtoto wa John Garang waliosimama mbele ya kamera za waandishi wa kimataifa kujaribu kuelekeza nini John Garang angependa kifanyike kinadhihirisha udhaifu wa SPLM. Kwamba SPLM ni John Garang na kinyume chake. SPLM ilikuwa ni chama mtu.
Naam. Kama kielelezo cha uimara na ubora wa chama chochote ni uwingi na ubora wa makada wake, basi kada bora ni nani? Katika chama kada hupikwa akaiva. Kada wa chama huwa tayari kununua na kupeperusha bendera mpya ya chama na kusahau kupaka rangi nyumba yake.
Siku zote kada hutanguliza maslahi ya chama yaliyojengeka katika misingi ya kiitikadi. Siku zote kabla ya kuamua ama kutenda jambo kada hujiuliza, je, jambo hili lina maslahi kwa chama changu? Je, jambo hili lina maslahi kwa nchi yangu? Ni kada wa staili hii anayesemwa amekunywa maji ya bendera!
Zamani watu walisema; "nakitumikia chama", mara nyingi walijitolea, waliacha kazi zenye nyadhifa na mapesa mengi, walibaki kukitumikia chama. Walijitolea na hata kujitoa mhanga kwa ajili ya chama. Siku hizi, kuna wanaoingia kwenye chama si kwa kukitumikia chama bali kutumikia nafsi zao. Hawako tayari kujitolea, wala kujitoa mhanga. Wanataka chama kijitolee na kujitoa mhanga kwa ajili yao! Wanataka uteule!
Naam. Kada bora hukielewa chama chake, hata umwamshe saa nane za usiku atakwambia madhumuni ya chama chake, kinasimama katika itikadi, malengo na shabaha gani. Kada katika chama ni kiongozi kwa namna moja au nyingine. Kuongoza ni kuonyesha njia. Unayemwambia sasa tunakwenda huku, ni lazima umweleweshe kwa nini tunakwenda huku. Kada wa chama si sawa kabisa na kamanda wa vijana katika chama.
Siku hizi tunasoma habari ya kuzuka kwa makamanda wa vijana wa vyama, CCM wanao watu kama hawa. Kuna makamanda wa vijana wa matawi, wilaya na kadhalika. Kada na kamanda ni vitu viwili tofauti. Kamanda ni msamiati wa kijeshi wenye kuambatana na amri na utii wa amri. Chama cha ukombozi kinaweza kuwa na makamanda, lakini makamanda hawana nafasi katika chama cha uongozi. Uongozi ni kuonyesha njia kwa nguvu za hoja na si kuamrisha njia ya kupita hata kama ina miba!
Nahofia kuwa , siku hizi, ukamanda umegeuzwa ngazi ya kupanda juu kisiasa. Naambiwa unaweza kuununua ukamanda wa vijana kwa fedha zako. Na hapa tunaona tufauti kubwa. Tunaweza kuwa na "kamanda wa vijana" asiye na vijana nyuma yake. Wanasimikwa ukamanda kutokana na unono wa mapochi yao au wana mahusihano na "wenye chama". Kamanda wa namna hii ukimwamsha saa nane ya usiku hawezi kwa uhakika akukupa idadi na majina ya vijana walio nyuma yake. Wako nyuma yake kwa misingi gani? Itikadi? Au wako nyuma wakishabikia pochi la kamanda? Huyo hafai kuwa kiongozi. Naam. Siasa si mchezo mchafu, kuna wanasiasa wachafu!
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home