MAKALA
Makala
miaka zaidi ya 45 tangu kupata uhuru, bado nchi nyingi za Afrika ni masikini wa kutupwa. Japo kuna utajiri mkubwa wa rasilimali tulizo zawadiwa na Mungu kama vile madini ya thamani, wanyamapori, ardhi kubwa yenye rutuba, misitu, samaki, bahari, milima na kila aina ya vivutio vya watalii. Lakini bado bara hili ni masikini. Tena umasikini mbaya ninaouna mimi ni ule wa fikra. Wahisani, wafadhili na wabia wa maendeleo wamemwaga mabilioni ya fedha kama misaada kwa Afrika kwa miaka mingi, lakini bado hali ni ngumu. Watu wa dini nao wamesali, wameomba na kufunga ili maendeleo yaje lakini umasikini ndio unakithiri. Mifumo ya Serikali imebadilishwa mara kadha ikiwemo ule wa vyama vingi vya siasa ili kujenga demokrasia na kuharakisha maendeleo Afrika. Lakini bado umasikini uko pale pale. Na tena unazidi kila siku. Tatizo ni nini? Chanzo nini ? Lini Afrika itapata maendeleo? Ulimwengu mzima unakubali kwamba daraja pekee la maendeleo katika nchi ni elimu. Pamoja na kuwa ukweli huu unajulikana hata hapa Afrika, kwa muda mwingi elimu hufanyiwa usanii na kupigiwa siasa tu. Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kuhusu dhana ya elimu. Viongozi wengi wa Serikali na watunga sera wanaitambua elimu kwa kuangalia takwimu za vitendea kazi kama vile madawati, wingi wa watoto darasani na hata majengo mazuri, basi wanaishia hapo! Wengine wanaitambua elimu kuwa ni kujua lugha za kigeni tu. Ndio maana hata wazazi wengi kwenye nchi za Afrika wanasifiwa elimu ya watoto wao kwa kuangalia uwezo wa mtoto kuongea Kiingereza au Kifaransa hata kama mtoto hajui kusoma wala kuandika. Hili lingekuwa hata na chembe ya ukweli basi nchi zinazoongea Kiingereza na Kifaransa zisingekuwa na haja ya shule maana tayari lugha zao ni elimu. Lakini kwa sababu lugha sio elimu nao wana shule na vyuo watoto wao wanapelekwa kupata elimu. Ukweli huu nahisi haujawahi kueleweka kwa Waafrika wengi. Sijui kwa nini! Bado, kwa muda mwingi elimu imechukuliwa kama ni utamaduni wa kizungu. Ndio maana Serikali zetu kwa miaka mingi wamepeleka Waafrika wengi kwenda kusoma Ulaya ili wakirudi wasaidie kuendeleza nchi zao kwa kuongoza fikra za ubunifu na kutumia maarifa waliyopata kubuni fursa na hata kuwapa maarifa wengine. Lakini wengi wamerudi na vyeti vingi, utamaduni wa kizungu na lugha za kizungu bila maarifa wala ujuzi wowote. Wamerudi wakapewa maofisi makubwa, magari ya kifahari, nyumba za kifahari na mishahara mikubwa inayotokana na kodi za Waafrika masikini. Badala wawe mstari wa mbele kuisadia jamii iendelee, wasomi hao ndio wamegeuka mzigo kwa Serikali na jamii na hivyo wamedidimiza maendeleo kwa kuligharimu Taifa. Wengi wamebaki wanajiita maprofesa huku kazi zao hazijawahi kuonekana. Wengine hata kuandika barua kwa mhariri ili watu wasome wapate maarifa hakuna. wameshindwa kuwaongoza wengine wapate maarifa au kubuni miradi ya maendeleo. Hakuna! Lakini wapo na wanataka kuheshimika sana. Tena wanatumia fedha nyingi kuuthamini na kuutunza utamaduni wa kigeni waliokuja nao kutoka Ughaibuni. Na wanakuwa viongozi wazuri wa kudharau utamaduni wetu, maadili yetu na mshikamano wetu wenye utu na umoja, ambao hata mataifa ya Ulaya mengine hayajawahi kufikia. Na kwa kukosa ubunifu, kamwe hawagusi vitu kwa mikono yao wanafanyiwa kila kitu. Wameweka watumishi wa kufanya kila kitu, nao wanalipwa na kodi za wananchi masikini. Wengine wamejipenyeza kwenye siasa na kushika madaraka makubwa serikalini. Kwa sababu wanashindwa kufikiri wala kuibua dhana mpya zitakazosaidia kuendeleza Afrika, Wanachofanya wanaamua kuuza kila rasirimali iliyoko nchini kwa jina la uwekezaji. Tena viongozi wengi hawatulii nchini mwao bali kila leo wako Ulaya kuomba fedha na kuwashawishi wakoloni tuliowafukuza miaka ya 1960 kurudi kupora rasirimali zetu. Je, hapa Afrika itaendelea kweli? Elimu ya namna hii kwanza haifai hata kuitwa elimu. Inafaa kuitwa utumwa wa kiakili na kiutamaduni. Japo ina madhara makubwa watawala wetu wanaing’ang'ania hasa kwa maslahi ya wachache. Tumefanya dhambi kubwa ya kuwarithisha hata watoto wetu elimu ya kujikataa na kukataa uafrika wao. Badala ya kuwapa maarifa na stadi za maisha zitakazo zaa wabunifu, watu wenye utashi mkubwa wa kuamua na kuunda vitu anuai. Bado tunawapa elimu ya cheti na utamaduni wa kigeni tu. Ni jambo la kushangaza kuona mtoto anahitimu shule anakimbilia mjini kuomba kazi ya ulinzi au kuwa mtumishi wa ndani. Wakati kwa kawaida ilibidi arudi kwenye familia yake na atumie ardhi kubwa ya baba yake na mifugo ya familia kufanya kilimo cha kisasa kutokana na maarifa na uwezo mkubwa wa kufikiri alioupata shuleni. Tunaona mtu na elimu yake yuko tayari kulipwa dola 50 kwa mwezi na hata kulala na njaa ili mradi tu abaki mjini. Kila siku tunawaona wasomi hadi wa shahada za uzamili wakilalama kwenye vyombo vya habari eti hawana ajira, wamesahau maarifa ndio ajira ya kwanza. Na rasilimali zinazowazunguka ndio daraja la maendeleo. Wakati huo wameacha rasirimali nyingi kijijini kwao zinazotamalaki tu. Rasilimali hizo kama wangekuwa na ubunifu na kujituma wangepata maendeleo makubwa kwa muda mfupi. Tena kama angepata maarifa shuleni angeweza kuzalisha mabilioni ya fedha kila mwezi kutokana na rasilimali za familia. Wengi wanageuka watoto wa vijiweni na pengine kuanza uvutaji wa bangi na kugeuka kuwa mzigo kwa jamii. Hivi ndivyo elimu ya sasa inavyowaandaa watoto wetu. Je, ni lini tutapata wabunifu? Ni lini magari, ndege, na vifaa kwa kisasa vitaundwa hapa hapa Afrika? Kuna faida gani kiongozi mmoja awe bilionea wakati wananchi wanabaki na shida nyingi wao na watoto wao? Ni dhambi nyekundu isiyosameheka. Tena viongozi hawa huapa kwa kutumia Biblia au Kurani wakati wa kukabidhiwa madaraka. Lakini wanachofanya ni kinyume na kilichoandikwa kwenye vitabu hivyo. Wanamsaliti hata Mungu wao. Hao ndio viongozi wengi wa Afrika. Watatoweka lini? Afrika ili iendelee sasa hatuhitaji fedha za wahisani. Tunahitaji elimu ya kweli. Elimu ambayo ina maana ya elimu na sio porojo za kisiasa au utamaduni wa kigeni. Elimu ile iliyoelezwa na wana falsafa kama Plato, Socrate, siku nyingi hata kabla ya kuzaliwa Kristo.Na elimu hiyo ni maarifa, ujuzi, uwezo wa kufikiri, makuzi ya utashi na hekima. Wangavu na upeo wa kuona mbali, uwezo wa kujitambua na kujithamini, uwezo wa kuthubutu, uwezo wa kuthamini kazi, uwezo wa kubuni fursa na kutumia fursa kujiletea maendeleo. Elimu yeyote lazima ilenge kumpa mtoto haya sio cheti wala utamaduni wa kizungu
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home