Tuesday, December 25, 2007

Kikwete, Sinclair na Barrick:Pembetatu ya machozi?


KWA mwaka mzima sasa hakuna kitu ambacho kimegusa hisia za umma wa Watanzania kama suala la madini.
Na kwa namna ya pekee suala hilo la madini lilifikia kilele chake pale mbunge kijana toka Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alipojikuta anapigwa “stop” kwenye Bunge baada ya kudai uundwaji wa Kamati teule ambayo ingechunguza mikataba ya madini na kuona kama “kuna sheria zilizovunjwa” na kuwatambua ni kina nani waliohusika.
Kitendo cha Wabunge wa CCM wakiongozwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waziri mkuu mstaafu John Malecela kumfungia kijana huyo kilisababisha si tu hisia ya uonevu, bali pia hisia ya ukandamizaji kwa kutumia nguvu ya Bunge.
Baadhi ya watu walionekana kukerwa na hali hiyo na wengine wakishikwa na madonge kooni ambayo yaliwafanya hata washindwe kusema. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu wananchi walishuhudia jinsi gani wingi wa wabunge wa chama kimoja bungeni unavyoweza kutumika vibaya kuhalalisha na kuficha mapungufu ya Serikali.
Siku zikapita na miezi ikenda; Na wananchi wakiwa wamekata tamaa Rais Jakaya Kikwete akatangaza kuwa ameunda tume ya ushauri juu ya sekta ya madini ambayo itaongozwa na aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa Tanzania Jaji Mark Bomani. Kuundwa kwa kamati hiyo kulipokewa kwa shangwe na baadhi ya watu hasa wale ambao ni mashabiki wa chama tawala wakiamini kuwa hatimaye “Rais kafanya kweli”. Na kwa watu wa kawaida habari hizo zilikuwa kama mvua iliyokuwa ikusubiliwa jangwani kwa miongo hasa pale kati ya wajumbe wake lilipotajwa jina la Zitto.
Hata hivyo, baada ya muda kupita na habari sahihi kutiririka, wananchi wakaambiwa kuwa Kamati hiyo si majibu ya hoja ya Zitto bungeni na kwa hakika “haihusiani moja kwa moja” na hoja hiyo ya Zitto.
Jaji Bomani mwenyewe akizungumza na mojawapo ya vyombo vya habari vya nje ya nchi alinukuliwa kukiri kuwa kamati hiyo kimsingi ni Kamati ya ushauri na haina nguvu za “kisheria” kama Kamati ya Bunge na hivyo haina uwezo wa kuita mashahidi au kuwalazimisha kisheria kusema ukweli au kutoa taarifa sahihi.
Wananchi wakiwa wanajikuna vichwa kufikiria mambo hayo wakaambiwa kuwa Kamati hiyo imeanza kuangalia kazi zilizofanywa na Kamati nne zilizotangulia kabla yake. Kwa mara ya kwanza (natumaini ni mara ya kwanza) ndani ya wiki chache Serikali ikaunda Kamati kuangalia kamati nyingine bila kuondoa uwezekano kuwa huko mbele kamati nyingine itaundwa kuangalia kazi za kamati iliyoundwa kuangalia kazi za Kamati nyingine! Watanzania waliokuwa wamejawa na matumaini kama walivyotumaini ushindi wa Taifa Stars, wakajikuta wamefungwa goli la kutolewa Challenji!
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete
Kitu kimoja ambacho Watanzania wengi hawajakifahamu au hakijawekwa hadharani inavyopasa ni sababu kubwa kwa nini Rais Kikwete hawezi na hatoweza kamwe kusafisha sekta ya madini nchini. Nia yake ya kutaka tuwe na kile anachokiita “win-win situation” haiwezi kukamilika na haitatokea kwa sababu yeye mwenyewe ni mdau kwa namna moja au nyingine na hali iliyopo sasa (status quo).
Hivyo wale wanaokaa wakiwa wanatumaini kuwa mapendekezo ya Kamati ijayo YOTE yatafanyiwa kazi na yatachangamkiwa, huyo bora ajiandae kukata tamaa na kushika tama. Kwanza kabisa mapendekezo yote hayatawekwa hadharani; kwa sababu ni mapendekezo tu na hiyo tume haitakiwi iyaweke mapendekezo yake hadharani bali kuyawasilisha kwa Rais kwanza na Rais halazimiki kuwaambia ni nini kimependekezwa.
Jambo la pili hata kama ataamua kutekeleza baadhi ya mapendekezo maslahi ya kwanza atakayoangalia na ambayo hadi hivi sasa ameyaangalia ni maslahi ya “wawekezaji” ili tusiwatishe. Hivyo mapendekezo yoyote ambayo kwa namna moja au nyingine yatatashia uwekezaji katika sekta ya madini yanakufa kabla hayajafika kwenye deski la Rais ofisini kwake.
Kwa kadiri Serikali ya Rais Kikwete inavyojaribu kutengeneza mizani ya mafanikio kati ya wawekezaji na wananchi kuwa ni lazima iwiane kwa hakika wanakuwa kama watwangao maji kwenye kinu. Je, ni lazima manufaa ya wawekezaji yalingane na manufaa ya wananchi wa nchi/maeneo ambapo wawekezaji wanafanya biashara zao?
Kwa kadiri ilivyo sasa inaonekana wazi kabisa kuwa wanaonufaika na uwekezaji ni makampuni na wananchi wanapata “viperemende” vya shule, zahanati n.k Je, yawezekana kupindua modeli hiyo na kuhakikisha kuwa mafanikio ya wananchi yanazidi yale ya makampuni?
Hata hivyo, kuna sababu nyingine na kubwa zaidi ambayo inamfanya Rais Kikwete kuwa na kigugumizi na wakati mwingine kusita kuchukua hatua za kijasiri, madhubuti, na zenye lengo kamili kuibadilisha sekta ya madini. Jambo hilo ni lile ambalo naweza kuliita ni pembetatu ya machozi. Pembetatu hii inamhusu Rais Kikwete mwenyewe, rafiki wa miaka 13 sasa James Sinclair, na kampuni kubwa kabisa ya uchimbaji dhahabu duniani ya Barrick Gold (kutoka Canada).
Kuweza kukaa chini na kuielewa pembetatu hii ndiyo mwanzo tu wa kuelewa ni kwa nini Rais Kikwete licha ya ahadi zake kuhusu mabadiliko katika sekta ya madini hawezi, hatoweza na hana sababu ya kuweza kubadilisha sekta hiyo ili iwe na manufaa zaidi kwa wananchi.
James Sinclair aliingia nchini akiwa na kampuni ya Sutton Resources na alianza shughuli zake za utafiti na uchunguzi wa madini. Baada ya kugongana na bodi ya wakurugenzi wa bodi hiyo Sinclair aliachana (alilazimishwa kuacha?) nayo na kuamua kuanzisha kampuni yake ya Tan Range Exploration iliyotokana na kampuni yake nyingine ya Tanzanian American Development.
Kampuni hii ya TRE liingia nchini ikiwa na lengo la kufanya ugunduzi wa madini mbalimbali (hasa dhahabu) na baadaye inapogundua eneo lenye madini hayo basi huliuza kwa makampuni makubwa ya uchimbaji madini na wao huanza kulipwa kiasi cha fedha kutokana na uchimbaji utakaofanywa pale. Kimsingi kampuni hiyo ya Sinclair haifanyi uchimbaji wa biashara bali wa utafiti na baadaye wakigundua madini basi hujitangaza kwa makampuni makubwa. Kampuni hii ina mikataba mbalimbali na baadhi ya makampuni na mkubwa zaidi ni ule kati yake na kampuni ya Barrick Gold ya Canada ambao wanaupendeleo maalum pale ambapo TRE wanagundua madini.
Akiwa na kampuni ya Sutton Resources Sinclair ndiye aliyesimamia utafiti wa eneo la machimbo ya Bulyanhulu ambayo kama wengi wanavyofahamu yanahusisha kuondolewa kwa nguvu kwa wachimbaji wadogo wadogo na madai ya kuwa baadhi yao walifukiwa wakiwa hai. Ni uhusiano huu ndio ulioifanya Sutton Resources kuuza machimbo hayo kwa Barrick Gold. Na kama nilivyosema hapo juu, kampuni yenyewe ya Sutton baadaye ikanunuliwa na Barrick.
Kuingia kwa Sinclair katika Tanzania kulikuwa kumepigiwa mahesabu ya kina na kubwa zaidi ni kujenga uhusiano wa karibu na wanasiasa na wadau wakubwa wa sekta ya madini. Yeye na binti yake, Marlene, wakaingia Tanzania mmoja akijenga uhusiano na wanasiasa na binti akijushughulisha na shughuli za kijamii. Lengo lao, hata hivyo, likiwa moja tu nalo ni kulainisha nyoyo za Watanzania ili hatimaye watakaposema wanachotaka wanapata.
Kuelewa upendeleo huu ni kuelewa kuwa wakati kampuni ya TRE inabadilishwa kutoka Tan Range kampuni ya Barrick Gold ilinunua hisa za mtaji kwenye kampuni hiyo mpya na hivyo kusaidia katika kuanza kwake. Pamoja na ushirikiano wa kibiashara na Barrick kampuni ya TRE ina ushirikiano na makampuni mengine ya uchimbaji ambayo yanafuatilia shughuli kwa uangalifu.
Leo hii TRE ni mojawapo ya makampuni/watu wachache wenye kumiliki eneo kubwa la ardhi. Ikiwa na leseni zaidi ya 120 za uchunguzi kuzunguka eneo la Ukanda wa Ziwa Victoria, kampuni hii kwa wengine inaonekana ndiyo kiini cha matatizo ya madini katika eneo hilo kubwa hasa kutokana uhusiano wake na kampuni ya Barrick Gold.
Kampuni ya Barrick Gold imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkubwa sehemu mbalimbali duniani kama Australia, Chile, Argentina, na Peru. Kitu kimoja ambacho hadi hivi sasa ni dhahiri ni kuwa kile ambacho Barrick inataka, Barrick inapata.
Katika kuhakikisha kuwa hilo linafanikiwa Tanzania, James Sinclair alijitahidi kuwa na urafiki wa karibu na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kati ya miaka ya 1990, Jakaya Kikwete. Kwa mujibu wa mmojawapo wa wasaidizi wa karibu wa Sinclair ukaribu wake na Waziri Kikwete ulijenga uhusiano wa karibu, kuaminiana na uwazi zaidi na matokeo yake ni urafiki ambao yeye mwenyewe Sinclair anauita ni wa “Karibu”. Urafiki huo ulidhihirishwa pale Rais Jakaya Kikwete alipomualika Sinclair katika sherehe za kuapishwa kwake!
Pembetatu hii inaendelea kuzunguka kila wakati na hasa hivi karibuni ambapo Rais Kikwete alirejea kutoka katika ziara yake ya “kikazi” ya ki Vasco Da Gama huko Marekani. Ziara hiyo ya Rais Kikwete ilitokana na mwaliko wa Mwenyekiti wa Bodi ya H. Sullivan Summit Balozi Andrew Young. Balozi Andrew Young ni mtu ambaye katika jamii ya watu Weusi wanamuona kama ni shujaa ambaye alishirikiana na marehemu Dk. Martin Luther, siku hizi ameanza kuonekana kwa mwanga mpya na tofauti.
Kuna baadhi ya watu ambao wanaamini kuwa Balozi Young amekuwa ni “mbeba mifuko ya ubepari wa Marekani” hasa kwenye nchi za Afrika. Imani ambayo imekuwa ikijengeka siku za karibuni kuwa Balozi Young amenunuliwa na anatumika kama kibaraka wa ubepari na hajali mambo mengine yoyote isipokuwa kutengeneza pesa kupitia migongo ya Waafrika.
Leo hii Andrew Young amepigia debe mkutano ujao wa Sullivan ufanyike nchini Tanzania jijini Arusha. Pamoja na sababu nyingi, bila ya shaka, Young atatengeneza ngawira kidogo. Kampuni ya Young inahusika moja kwa moja na umiliki wa hoteli ya Mt. Meru mjini Arusha.
Lakini zaidi ya yote, Young ni mjumbe wa bodi ya Ushauri ya kampuni ya Barrick Gold. Hivyo bila ya shaka uhusiano wake wa karibu na Rais Kikwete, Waziri wa Madini Nazir Karamagi, Sinclair na watu wa Barrick unamsaidia sana katika kuhakikisha kuwa mambo hayaendi vibaya kwa Barrick hasa yanapokuja kwenye maamuzi ya Serikali.
Kwa kuangalia mambo hayo tunaweza kuona pembetatu ambayo ndani yake kuna mambo mengi ambayo kwa hakika yameshikamana na kufuatana kama lila na fila. Tunaweza kuona jambo moja dhahiri kuwa Rais Kikwete, Kamaragi, James Sinclair, na Andrew Young wote wanaunganishwa kwa namna moja au nyingine na kampuni kubwa kabisa ya madini duniani ya Barrick Gold. Na tukiangalia mifano ya nchi mbalimbali ambako Barrick imekuwa ikilalamikiwa na kupata upinzani tunaona kuwa Barrick haiko katika upande wa kushindwa.
Hakuna sheria au taratibu ambazo zinaweza kutengenezwa na nchi yoyote inayoendelea ambazo zinaweza kuweka matatani maslahi ya kampuni hiyo kubwa ya madini. Kile ambacho Barrick inataka, Barrick inapata.
Kwa kuangalia ukweli huo basi ni wazi kuwa kikwazo kikubwa cha mabadiliko katika sekta ya madini itakuwa ni kampuni hiyo kwani wao wakigoma hakuna kitakachofanyika. Ndiyo maana kutokana na pembetatu hiyo ilikuwa ni rahisi kuishawishi kampuni hiyo kubadili baadhi ya vipengele vya mikataba yake kiasi cha kwamba walikuwa ni wa kwanza kutangaza “kukubali” mapendekezo ya Serikali (ambayo wao wana uhusiano wa karibu nao).
Pembetatu hii kwa hakika imesababisha Watanzania walie sana mwaka huu unaoisha na sitashangaa wakawa tena sababu ya machozi zaidi mwaka ujao. Rais Kikwete hana ubavu wa kusimama mbele ya kampuni kubwa kama hii hata kama atapata ushirikiano kutoka kwa wananchi. Barrick imekuwa ikitamalaki sehemu mbalimbali duniani licha ya pingamizi toka kwa watu mbalimbali.
Ndiyo maana watu kama kina Tundu Lissu wanavyojitahidi kupambana na kampuni hii wanakuwa wamejiweka katika kundi la kushindwa. Tundu Lissu hana ubavu wa kupambana na kampuni iliyozungukwa na pembetatu hii. Kamati ya Madini ya Bomani haina ubavu huo pia kwani haina nguvu zozote na Rais Kikwete alijua ni kwa nini hakutaka iundwe kamati Teule ya Bunge isipokuwa kamati ya ushauri tu; ushauri ambao watekelezaji wake wakubwa watakuwa ni Barrick Gold.
Ni kwa sababu hiyo basi yeyote ambaye amekaa kwa moyo wa matumaini kuwa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya madini huko tunakokwenda yuko njozini. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana hadi leo Serikali imeshindwa kutoa hadharani ripoti za Dk. Kipokola, Mang’enya, Jenerali Robert Mboma na Laurence Masha.
Kwa sababu mapendekezo hayo hayakukubaliwa na “wakubwa”. Hata mapendekezo ya kamati ya kina Zitto ambayo ninaamini yatakuwa mazuri sana yatatupwa nje kama takataka chafu kwani Barrick haiwezi kufanya katika Tanzania kile ambacho imekataa kufanya nchi nyingine.

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home