Kwako Mwalimu Julius Nyerere
NINAKUANDIKIA kukutaarifu kuwa tumemaliza mwaka 2007. Na sasa ni mwaka 2008. Mwaka uliopita, yaani 2007, ulikuwa na vimbwaga vingi sana.
Napenda nianzie na nyumbani kwako. Mwanao, Madaraka Nyerere, anapambana kweli kweli kutukumbusha kwamba Butiama ipo. Kila Jumapili anaandika makala, na makala hizo anaziita: Waraka kutoka Butiama ama “A letter from Butiama” kwa Kiingereza.
Tatizo ni kwamba sina hakika kama watu wengi wanaziona hizo barua zake kutoka Butiama, kwani siku hizi magazeti anakoandika, na mengine, yale uliyoyaanzisha wewe, mtu akikuona unayasoma anakushangaa kweli kweli.
Mwanao mwingine, yule ambaye wakati fulani alijiunga na Mageuzi, lakini akarejea, Makongoro, amekuwa chifu wa Mkoa wa Mara. Sasa ni Mwenyekiti wa chama tawala yaani CCM wa Mkoa. Sijui kwa nini amekataa cheo chake kuwa chifu na akapenda kuitwa mwenyekiti.
Tetesi zilizopo ni kuwa wale Wazanaki na wenzao wa kure Mara walikataa asitumie neno hilo chifu kwa sababu yeye ana mke mmoja tu. Na hawezi kuthubutu kuongeza mke mwingine, kwani mkewe, yaani mkweo, sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu.
Mwanzoni mwanzoni mwa mwaka uliopita walikuzushia maneno huku, kuwa wewe ulikuwa na hekalu pale Magomeni, Dar es Salaam . Hekalu hilo linataka kuvunjwa ili pajengwe jengo kubwa la kupangisha. Yakapangwa maandamo kukutetea. Mama Maria, na Makongoro wakatoka huko walikokuwa, wakali kweli kweli, wakaweka mambo sawa. Maandamano yakafa. Si ni kweli pale Magomeni ulikaa kama mpangaji eti?
Nadhani mengine, ya ndani zaidi, amekuletea Kiboko Nyerere maana aliondoka huku ghafula na hatumuoni tena siku hizi.
Tanzania yako ipo, na wanaokuenzi wapo. Wanakuenzi kwa maneno, kwa matendo na kwa kutotimiza wajibu. Kilimo ambacho ndio uti wa mgogo kipo kama alivyokiacha Adamu na Hawa. Hakuna wa kukisemea. Wote wanakodolea macho madini. Mwalimu; madini yamekuwa madini.
Utakumbuka kuwa ulianzisha Stamico, haisikiki kabisa. Nadhani nayo ilikufa. Si ajabu wale walioiuwa ni miongoni mwa wale wanaopiga kelele kuwa madini yetu yanachimbwa na wageni.
Utakumbuka pia wakati unaishi Waswahili hawa walikuwa wakichimba dhahabu na soko lao la dunia lilikuwa pale kuvuka kidogo Sirari, lakini upande wa Kenya? Waswahili wale wakaifanya Kenya kuwa muuzaji mkubwa wa dhahabu kwenye soko la kweli la dunia.
Utakumbuka kuwa wakati ukiwapo, sikumbuki kama wakati huo tulikwisha kuanza kukuita Baba wa Taifa, kaliletwa kautaratibu ka Benki Kuu kununua dhahabu. Waswahili badala ya kupeleka dhahabu wakayeyusha mabirika na chochote chenye rangi ya dhahabu wakauza pale Benki Kuu. Wakachukua fedha yote na mradi ukafa. Nao sasa wanapinga kelele kuwa dhahabu inaibwa. Sijui ni vipi Mwalimu, maana kama wangejua dhahabu ipo na ni gharama nafuu kuitafuta na kuichimba kwa nini waiuzie Benki Kuu myeyusho wa mabirika?
Mwishoni mwa mwaka jana CCM walifanya uchaguzi, wakachaguliwa viongozi . Sasa wanajipanga kuhakikisha wanabaki Dar es Salaam, si Dodoma uliyopendekeza wewe. Waswahili hawa wanadhani ulipendekeza Dodoma ndiyo iwe Dar es Salaam kwa sababu ya Vita Baridi, ambayo kweli imeisha. Wanasahau kuwa sababu ya kwanza ilikuwa Dodoma ni katitikati ya nchi hata yule King Kiki na Double O yake anajua hivyo.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wapo Waswahili wa kwao Sir George Kahama na ka kundi kanakoitwa REDET. Mwaka 2005 walifanya tathimini. Wakasema mgombea wa CCM angeshinda urais kwa zaidi ya 80 %. CCM wakafurahi kweli na wapinzani wakaiita tathimini yao maneno ya magengeni.
Hivi karibuni REDET wakaibuka tena na maneno wakasema zikipigwa kura leo yule aliyepata 80% atapata chini sana ya hizo. Kisa? Yeye akivuta wenzake wanasimama tu. Looh! CCM wakanuna, na wale watani wao wakasema REDET poa!
Hali ya maisha mwaka huu tuliouanza kwa kweli itakuwa ngumu kweli. Ndiyo. Kwani tukianzia nyumbani tu yaya ujira wake anatakiwa apate shilingi 65,000. umeme unapanda, kumbe Tanesco wametulemaza kweli. Kaja jamaa mmoja pale haelewi. Kakuta Waswahili kama nguzo wanainunua kwa Sh. 210,000 wao wanaiuza kwa Sh. 90,000. Akasema stop. Koleo liitwe koleo. Sasa tumegeuzwa. Nina hakika tumegeuka mawe.
Uliopondoka uliahidi kuwa unatupenda na utatuombea kwa Mungu sisi Watanzania wako. Ninaomba utuombee tupate neema ya kuishi maisha halisi na si ya kununua cha 200 kwa 50.
Mafuta yale yaliyokupa tabu baada ya kumtoa Amin, sasa ni balaa tupu. OPEC, wale wanapandisha bei kutwa mara tatu. Rafiki zako Wachina wanaula sasa wanatengeneza kila kitu. Na Watanzania wako siku hizi tunakwenda huko kama tulivyokuwa tunaenda Kisumu enzi zako.
Lakini kuna tofauti kidogo, wakati Kisumu tulikuwa tunapeleka ngozi, tunauza ngozi , tunapata fedha za Kenyatta, hivi yupo? Msalimie. Kisha tunanunua Empriel leather ya kweli, Waswahili wanaokwenda China wanakwenda na dola zetu Mwalimu, wanatuletea bidhaa feki. Lakini feki hii ya sasa haina maana sawa na bandia, maana yake ni bidhaa kulingana na uwezo wa mnunuzi.
Mwalimu mwambie Kenyatta na pia mnong’oneze Jaramogi Odinga kuwa Kenya bado iko vilevile. Mjaluo kuwa rais haiwezekani. Pia Bhuto baba na Bhuto mtoto kuwa Bhuto mjukuu na Butho mtoto sasa ndiye rais wa chama chao.
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home