Monday, January 14, 2008

Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya Mapinduzi

VISIWA vya Zanzibar vilipata uhuru wa bendera Desemba 10, 1963 kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika Julai 8-15, 1963 pale muungano wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People`s Party (ZNPP)-ZNP/ZNPP ulipoibuka mshindi kwa viti 18 katika Bunge dhidi ya viti 13 vya chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).

Kwa ushindi huo, Mohamed Shamte wa ZPPP aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Zanzibar na Sultan wa Zanzibar Jamshid bin Abdallah Khalfa Harubu alibakia kama Mkuu wa nchi, mwenye mamlaka ya kuteua mrithi (Gazeti la serikali 1963).

Kilichoshangaza ulimwengu ni jinsi Serikali ya Shamte ilivyopinduliwa hima, siku 34 tu toka uhuru wa bendera, yaani Januari 12, 1964 katika mabadiliko sawia ambayo wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanayaeleza kuwa ni ya aina yake katika nchi za Kiafrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukiondoa Guinea ya enzi za Rais Sekou Toure. Nini na kina nani ‘waliochochea’ mapinduzi hayo?

Wakati kuna majibu ya kutosha juu ya sababu ya Mapinduzi hayo, bado ni kitendawili ni nani aliyaanzisha na kuyaongoza kiasi kwamba suala hili limepata simulizi na tafsiri mbalimbali zinazokinzana na kuacha umma gizani.

Katika makala haya kwa kutumia vyanzo mbalimbali tutaelezea matukio yaa kabla, wakati na baada ya Mapinduzi, kuwawezesha wasomaji kupata angalau picha ya nini kilichotokea ili kuweza kujibu swali “nini na nani alichochea au kuongoza Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo sherehe za miaka 44 ya kumbukumbu yake zinafanyika Jumamosi hii.

Harakati za uhuru Zanzibar kwa sehemu kubwa ziliendeshwa na vyama vikuu viwili –ZNP kilichoundwa Desemba 1955 na ASP kilichoanzishwa Februari 5, 1957.

Kati ya mwaka 1959 na 1963 kuelekea uchaguzi wa Julai 1963, mitafaruku ilizuka miongoni mwa wanaharakati wa vyama hivyo, Mohamed Shante akijiengua kutoka ASP na kuunda chama cha ZPPP ambapo Abdulrahman Mohamed Babu alijitoa ZNP na kuunda Umma Party (UP) chama cha mrengo wa kushoto.

Katika uchaguzi wa Julai 1961, ASP kilipata asilimia 49.9 ya kura zote, ZNP kilipata asilimia 35 na ZPPP asilimia 13.7. Hata hivyo, pamoja na ushindi wa kura ASP, kilishindwa kutamba katika viti vya bunge (LEGCO) kilipopata viti 10, ZNP 10 na ZPPP vitatu.

Uchaguzi huo ambao haukupata mshindi na ulifuatiwa na ghasia, zilizoacha watu 68 wakiuawa na wengine 400 wakiwa majeruhi. Watu 100 walikamatwa hivyo ilibidi urudiwe Julai, 1963, chini ya ulinzi mkali wa askari zaidi ya 100 waliwamo askari wa Kiingereza.



WAZIRI Mkuu Shamte na baraza lake la mawaziri lililopinduliwa.

Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa kama ifuatavyo muungano wa ZNP/ZPPP viti 18 na ASP viti 13 chama cha umma hakikugombea. Shamte alishauriwa aunde Serikali ya mseto kati ya ZNP/ZPPP na ASP ili kulinda umoja wa kimataifa, lakini alikataa kwa kiburi kwamba hawezi kukubali “kugawana mateka”

Sherehe za uhuru zilifanyika Desemba 9, 1961 zikihudhuriwa na watu mbalimbali mashuhuri kutoka nchi 70, akiwamo mwana wa Mfalme (Duke) wa Edinburgh pamoja na Aga Khan. Hakuna kiongozi yeyote wa Afrika aliyehudhuria.

Katika salamu zake za uhuru siku hiyo, Babu wa Umma Party aliwashangaza watu alipomaliza kwa kusema “umma wa Zanzibar na chama chao cha UMMA unasubiri kunyakua madaraka ya nchi saa itakapowadia”. Alikuwa na maana gani?

Serikali ya Shamte ilitoa haraka haraka madaraka makubwa kwa Wazanzibar katika Jeshi la Polisi, ambayo kabla ya hapo yalishikwa zaidi na Wamakonde kutoka Tanganyika na Msumbiji Kaskazini, ambao sasa waliachishwa kazi na kubakia Visiwani kwa uchungu bila kazi.

Mapema Januari 1964 (kabla ya Mapinduzi) Serikali ya Shamte ilikipiga marufuku chama cha UMMA na Babu akawa anasakwa kwa kosa la uhaini kwa kuhutubia mkutano wiki mbili kabla na kumshambulia Sultan na Serikali ya “kibaraka” Shamte. Kwa sababu hiyo alikimbilia Dar es Salaam kukwepa kukamatwa.

Tetesi za Mapinduzi zilianza asubuhi Jumamosi ya Januari 11,1964 ambapo Sultan Jamshid alidokezwa uvumi kwamba kungetokea machafuko siku hiyo usiku au kesho yake lakini kwa kuhakikishwa na waziri wa usalama kwamba huo ulikuwa ni uvumi usio namsingi aliamua kuupuuza.

Jioni ya siku hiyo askri wa kuzuia fujo Kambi ya Mtoni walipewa amri kwenda kuzuia fujo mjini Unguja umbali wa kilomita tatu wakabakia huko usiku huo. Ndipo vikundi vya wananchi viliposhambulia na kuteka Kituo cha Polisi cha Ziwani na kujipatia silaha na hatimaye kushambulia Kituo cha Mtoni kwa uraisi na kuteka silaha nyingi zaidi.

Hadi saa 11.00 alfajiri Vituo vya Ziwani na Mtoni vilikuwa vimesalimu amri, upinzani pekee ukibaki Kituo cha Malindi karibu na bandari ya Unguja.

Wakati huo huo Shamte aliendelea kutapatapa kuomba Uingereza ipeleke majeshi, lakini ombi hilo likakataliwa kwa sababu nchi hiyo haikuwa na mkataba wa ulinzi na Zanzibar. Alitumia ndege ndogo Pemba kuleta silaha lakini ilishindikana kurejea baada ya Uwanja wa Zanzibar kufungwa.

Saa 3.00 asubuhi Sultan Jamshind alitaarifiwa na watu wake kuwa majeshi ya Serikali yalikuwa yameshindwa na kwamba aondoke Zanzibar katika muda wa dakika 10.

Kwa kutumia ulinzi wa Kituo cha Malindi, Jamshid alitoroka jumba la kifalme akaingia kwenye boti iendayo kasi iliyoitwa Salama na kuingia kwenye meli “Seyyid Khalfa” kwenda Mombasa kutafuta hifadhi, lakini Serikali ya Kenya ikamkalia, akageuza njia kuelekea Dar es Salaam.

Siku hiyo ya Jumapili ambayo ndiyo ilikuwa siku kwanza ya Mapinduzi machafuko yaliendelea hadi mashambani kwa walalahoi kuwashambulia mamwinyi.

Siku ya kwanza; Jumapili Januari 12:

Asubuhi uvumi ulienea kwamba Mapinduzi yaliendeshwa na vyama vya UMMA na ASP, kwamba UMMA waliratibu oparesheni yote na ASP walitoa askari. Uvumi huo ulisema vijana wa Babu wanashirikiana na washauri kutoka Cuba.




"Field Marshal" John Okello na wanamapinduzi wenzake.

Jioni ya siku hiyo, mtu mmoja mwenye sauti nzito, alitangaza kwa Kiswahili kupitia Radio Zanzibar na kujitambulisha (bila kutaja jina) kama “Field Marshal” alisema “sasa Zanzibar ni Jamhuri, vyama vya ASP na UMMA vitaunda Serikali mpya, Rais atakuwa Sheikh Abeid Amani Karume”. Katika hali ya kukanganya aliita kwa sauti ya kuamrisha “Karume (popote ulipo) rudi haraka kuchukua nafasi yako”

Inasemekana Karume aliondoka Dar es salaam siku ya Jumamosi kabla ya Mapinduzi kuanza au kushika kasi kwa madai ya kwenda kumweleza Mwalimu Julius Nyerer jinsi Mapinduzi yanavyofanyika na kufuatiwa na Kassim Hanga siku ya Jumapili asubuhi kwa madai ya kwenda kupata bunduki zaidi.

Itakumbukwa kuwa kwamba Babu wa UMMA alikuwa Dar es Salaam tangu alipotoroka huko kukwepa kukamatwa sasa kama wote hawa hawakuweao Zanzibar nani aliongoza Mapinduzi?

Kitu kingine kinachoshangazaa wengi ni kuwa katika orodha ya wajumbe 30 wa Baraza la Mapinduzi iliyotolewa baadaye jina la Okello ni la kwanza lakini Karume halikuwapo hata miongoni mwa majina ya wajumbe 14 wa Kamati ya Mapinduzi (Gazeti la Serikali , Januari 25, 1964).

Usiku siku hiyo Mwalimu Nyerere alionana na Karume Ikulu na kumshauri arudi Zanzibar mara moja baada ya kuona hapakuwa na sababu ya yeye kuwa Dar es Salaam.

Siku ya pili; Jumatatu Januari 13:

Asubuhi “Field Marshal”alijitambulisha kama kawaida kupitia redioni kwa jina la John Okello kisha kwa sauti yenye mamlaka akaendelea kusema: “Sultan amefukuzwa mguu wake hautakanyaga tena ardhi yetu, jumba lake na mali yake itataifishwa” kisha akaiomba Serikali ya Tanganyika ipeleke ndege nzima ya dawa na kuwataka wauguzi wote warudi kazini.

Aliendelea kutamba: “Nitachukua hatua kali, kali mara 88 zaidi, hakuna ruhusa mtu kuacha mke wake atakayefanya hivyo atapata viboko 65; Sultan alikuwa shetani na kibaraka wa mabepari. Mtu atakayejaribu kuwa mnafiki atafungwa miaka 50, atakayeiba hata mche wa sabuni atafungwa miaka minane. Mimi ni Field Marshal naweza kutengeneza mabomu 800 kwa saa moja”

Siku hiyo mchana, Oscar Kambona, Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Tanganyika, alimpigia simu Rais Nyerere kutoka Nairobi kumjulisha kuwa Kenya na Uganda zimeitambua Serikali ya Mapinduzi na kumwomba aitambue pia bila kumeza maneno Nyerere alikataa kwa kuwa hakuwa na hakika kwamba Karume na ASP walikuwa wameshika hatamu na kwamba hakuyapendelea mauaji yaliyokuwa yakiendelea.

Kwa mujibu wa Okello baadaye alieleza kuwa watu 9,999 waliuwawa lakini kulikuwa na taarifa nyingine za kuwa walikuwa ni 200, japo taarifa za Mzungu mmoja Visiwani zilikadiria watu 6,000 kuwa waliuawa.

Vivyo hivyo katika simu hiyo Kambona alimjurisha Nyerere juu ya Sultan Jamshid kukataliwa kutia nanga Mombasa na kumshauri naye asimruhusu, hata hivyo, Nyerere alimjibu Kambona kuwa hakuwa na ugomvi na Sultan, kwa hiyo, hakuwa na sababu ya kutomruhusu nchini.



KARUME na John Okello

Karume na Hanga waliondoka Dar es salaam kutokea eneo la “Silver Sands” saa 8.00 alfajiri (saa 24 baada ya Mapinduzi kwanza) kuelekea Zanzibar kwa boti ya Fainzilber na kufika Zanzibar saa 6.30 baadaye eneo la Kizimkazi asubuhi ya Jumanne waliomba na kupata usafiri wa gari la mwalimu mmoja wa shule na kwenda moja kwa moja eneo la Raha Leo na kulakiwa na “Field Marshal” wakala chakula pamoja.

Siku ya tatu; Jumanne Januari 14:

“Field Marshal” John Okello alitangaza kupitia redio kwamba mawaziri wanne wa Serikali ya zamani watanyongwa, lakini Karume alipinga siku iliyofuata (Januari 15) kwamba hakutakuwepo kulipiza kisasi.

Siku hiyo Mwalimu Nyerere alikwenda Nairobi kuonana na Waziri Mkuu wa Kenya, Jomo Kenyatta, kuzungumzia uundwaji wa shirikisho la nchi za Afrika Mashariki. Ni katika ziara hiyo Mwalimu alipoanza kubaini kwamba Jomo Kenyatta hakuwa na shauku ya kuundwa kwa shirikisho hilo ambalo ndoto yake haijatokea kuwa ya kweli hadi leo.

Siku ya nne; Jumatano Januari 15:

Sultan Jamshid aliyekataliwa kutia nanga Mombasa na Serikali ya Kenya alitia nanga Dar es Salaam na kuruhusiwa na Mwalimu Nyerere kukaa nchini hadi alipokamilisha mipango yake ya kukimbilia uhamishoni Uingereza siku nne baadaye.

Siku ya tano Alhamisi Januari 16:

Huku “Field Mashal” Okello akiendelea kutoa matangazo mbalimbali kupitia radio, Karume, Babu na Hanga waliondoka kwa ndege kwenda kuonana na Nyerere kumwomba aitambue Serikali yao na kuomba askari wachache kuweza kurejesha amani na utulivu Visiwani. Siku mbili baadaye askari 300 waliwasili Zanzibar.

Okello pengine bila kufahamu juu ya safari ya Karume, Babu na Hanga, alitangaza redioni kulalamika kwamba alifanya makosa kumteua Karume kuwa Rais kwa sababu hakushiriki hata kidogo katika mapambano, hivyo siku hiyo, Okello alijipa mwenyewe cheo cha Rais na kumtangaza Karume kuwa makamu wake.

Mchana “Field Marshal” Okello alitembelea makao makuu yake yaliyokuwa kwenye Jumba la Manjano, Raha Leo ambako umati mkubwa wa watu ulikuwa ukimsubiri kumwona akiwa amevaa mavazi meusi ya kijeshi, mara alipojitokeza tu umati ulizizima kwa shangwe na kupiga kelele “Jamhuri! Jamhuri!.......”

Siku hiyo Okello alikaribisha wageni wa kimataifa na kwa msaada wa mkalimani alizungumza kwa kirefu habari za maisha yake na jinsi alivyopanga Mapinduzi ya Januari 12 bila kumwambia Karume wa sababu angeyazuia kutokana na ukweli kwamba bado alikuwa na matumaini ya kufika mwafaka na Shamte wa kuunda serikali ya mseto.

Huko nyuma Karume alimtumia Shamte ujumbe mara mbili kumbebeleza akubali lakini Shamte alikataa kata kata akitaka ASP kivunjwe.

Siku ya nane; Jumapili Januari 19:

Siku ya sita na ya saba, Okello aliendelea kutangazia umma juu ya Mapinduzi na matarajio yake kama kawaida lakini siku ya nane aliondoka kwenda Dar es Salaam kama mapumziko kidogo baada ya kazi kubwa. Usiku huo alionana na Mwalimu Nyerere Ikulu na alishauriwa kufanya kazi kwa imani na Rais Karume. Aliporejea Zanzibar siku moja baadaye aliambiwa anatakiwa Dar es Salaam. Nyerere alimkamata Uwanja wa Ndege wa Dar es salaam na kurejeshwa kwao Uganda.




John Okello akiwa chini ya ulinzi

Kwa hiyo wanaharakati hawakuyatambua matokeo ya uchaguzi wa 1961 na 1963 na kwamba ASP kilidai kupokonywa ushindi. Lakini swali juu ya nani aliongoza Mapinduzi ya Januari 12 halijapata jibu.

Tunaambiwa kuwa ni Mzee Karume aliyeongoza mapambano, lakini hoja hii imejaa ukingu baridi na maswali tele kwa nini alikimbilia Dar es Salaam kabla au mara Mapinduzi. Kama ilikuwa ni kumjulisha Mwalimu Nyerere juu ya Mapinduzi kama alivyodai kwa nini asingepiga simu?

Kwa nini Nyerere hakuyatambua Mapinduzi mapema na kwa haraka kama zilivyofanya Kenya na Uganda? Kwa nini alimhifadhi Sultan Jamshid kwa chukizo la Karume na wanamapinduzi? Kuundwa kwa serikali ya mseto kati ya ASP na Umma kunaonyesha nini juu ya Mapinduzi? Na kama tutakataa kwamba Okello ndiye aliyeongoza Mapinduzi kwa nini aliruhusiwa “kutamba” kwenye radio ya Serikali (mpya) kwa siku nane mfululizo?

Na kama tutakubali kuwa Okello ndiye aliyeongoza na hatimaye Karume (ASP) na Babu (Umma) wakaunda serikali ya mseto Karume akiwa rais na “Field Marshal “ John Okello akatupwa nje; je, tuseme hatua hiyo yalikuwa Mapinduzi ndani ya Mapinduzi?

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home