Tuesday, December 25, 2007

Maximo hapaswi kulaumiwa


TIMU ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars
TIMU ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars Jumatatu wiki ilitolewa katika michuano ya Kombe la Challenge baaada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sudan katika mchezo wa robo fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa zamani wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo hayakupokewa vizuri na mashabiki waliofurika kwenye uwanja huo ambao walikuwa na matarajio makubwa ya Bara kusonga mbele kufika mbali au kutwaa kombe kama ilivyowahi kufanya katika miaka ya nyuma ikiwa mwenyeji.
TIMU ya soka ya taifa la Sudan
Kama mwenyeji imetolewa mapema zaidi mwaka huu kwani mwaka 1975 baada ya kufika fainali na kutwaa kombe mbele ya Uganda, mwaka 1992 ilifungwa katika mchezo wa fainali na Kenya baada ya timu yake wa pili ya Kakakuona kuwashangaza wengi kwa kufikia hatua hiyo.
Mara ya mwisho pia ilikata mbunga na kufika fainali na kufungwa na Kenya kwa mabao 3-0.
Mwaka huu matumaini yalikuwa makubwa kwamba timu hiyo itafika mbali hivyo kuboresha rekodi yake ya kushiriki mashindano hayo kwani mara ya mwisho ilitwaa kombe hilo mjini Nairobi mwaka 1994.
Je, ni wapi ambako timu hiyo imejikwaa kiasi cha kutolewa mapema zaidi nyumbani licha ya kushindwa kuboresha rekodi ya kutwaa kwa mara ya mwisho mwaka 1994.
Sasa, baada ya matokeo haya, mengi yatasemwa. Tayari eneo zima la Uwanja wa Taifa lilichimbika baada ya mpira kumalizika baada ya baadhi ya mashabiki kuja juu kumzomea Maximo na hata kulirushia mawe basi la wachezaji.
Askari Polisi wa kutuliza ghasia (FFU), walilazimika kuingilia kati kutuliza ghasi kwa kufyatua mabomu ya kutoa machozi.
Je, Maximo kweli anastahili lawama kwa matokeo hayo? Kama si Maximo ni wachezaji wenyewe au Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kwa kushindwa kuandaa mazingira mazuri ya ushindi?
Haya ni maswali ya kujiuliza. Lakini, kabla ya kujibu swali lolote kati ya hayo ni muhimu kufahamu kwamba tunazungumza michezo hapa na katika mchezo wa soka kama ilivyo mingine mingi, kuna kushinda, kushindwa na kutoka sare.
Kwa maneno mengine ni kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani. Kocha Maximo baada ya mchezo huo alikubali matokeo ya kushindwa alipozungumza na waandishi wa habari waliomzunguka.
Baadhi ya mashabiki wa soka nchini wanamlaumu kocha huyo kwa kuingiza kikosi kipya kwenye michuano hiyo, si kile ambacho alihangaika nacho wakati anataka kuiduwaza dunia kwa kuiondoa Senegal katika michuano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Ghana mwakani.

Soka la sasa limebadilika mno. Si lile la ‘fulani ana mpira, fulani ana mpira’ au la kuingiza uwanjani ‘majina yanayotisha’ yanayochezea klabu fulani na fulani zenye umaarufu mkubwa.
Umri na uwezo wa kucheza mpira ni vitu viwili vinavyozingatiwa mno na makocha wa siku hizi. Kwa bahati mbaya, Maximo anaonekana kama anabahatisha kwa sababu amekuta nchi hii halina soka la vijana, Wizara ya Elimu chini ya Joseph Mungai ilikwishaua soka hiyo kwa kuondoa michezo ya shule za msingi na sekondari.
Michuano mikubwa ya kimataifa iliyoko mbele yetu ni ile ya kufuzu kucheza fainali za Dunia 2010 zitakazofanyika Afrika Kusini.
Wengi wa wachezaji waliokuwa wanapikwa na Maximo mwaka jana na mwaka huu kwa ajili ya fainali za Ghana watakuwa wengi wao ‘wanamalizia’ mpira wao wakati kindumbwendumbwe cha 2010.
Kocha anayeona mbali ni lazima aanze sasa kuwaaanda vijana ambao anaona watakuwa na msaada mkubwa kwa kipute cha kuwania tiketi ya Afrika Kusini.
Katika hali hiyo basi, alilazimika kuita kikosi kilichosheheni yosso wengi kwa ajili ya michuano ya Challenge ambayo mbio za timu hiyo zimekwamia kwa Sudan.
Maximo hakuwa kocha pekee aliyokuwa na mawazo hayo katika michuano ya mwaka huu ya Challenge. Kenya ilikuwa na timu kama hiyo na bila shaka na nchi hiyo inataka kufanya kama Maximo anavyotaka kufanya.
Katika ‘akili’ ya zamani, kocha wa Sudan angeleta ‘full muziki’ wa kikosi atakachokitumia Ghana mwakani baada ya timu ya nchi hiyo kufuzu kucheza fainali hizo.
Pamoja na ukweli kwamba michuano ya Challenge ilikuwa ni uwanja mzuri wa kuwapima wachezaji wake kwa fainali za Ghana, hakutegemea wachezaji wale tu walioiwezesha timu hiyo ifuze kwenda Ghana.
Hata kocha wa Sudan ameleta kikosi chenye yosso wengi. Kutokana na mashindano hayo, kikosi chake kitakachocheza Ghana kitakuwa na mabadiliko makubwa baada ya kuvishuhudia vipaji vipya vilivyochomoza katika mashindano haya ya Challenge.
Ingawa ni kweli tulielekeza macho yetu Ghana, lakini tukashindwa na sasa tumeelekeza macho yetu Afrika Kusini, ukweli ni kwamba tumo katika hatua ya kulijenga soka letu ambalo lilikuwa limelala kwa sababu kutokuwa na mwamko wa kuwa na timu za vijana.
Nani amewasahau Watoto wa Yanga, Simba na timu ya UMISSETA wa mwaka 1980? Makundi ya timu hizo ndiyo yaliyokuwa yamefanya baadaye soka la Tanzania kuwika.
Yanga na Simba wakati fulani kuwa na timu B kulisaidia pia kupandisha soka kwa kuwa na vijana wengi wanaolilia namba ya kucheza si kulilia pesa za kusajiliwa.
Mfano mzuri ni Madaraka Selemani aliyestaafu soka akiwa bado tishio. Baada ya kulilia namba bila mafanikio kwenye kikosi A cha Simba, Madaraka alijiondoa Simba B kwenda mikoani na kurudi Simba kwa ‘gharama’ kubwa.
Roma haikujengwa kwa siku moja. Mashabiki wa soka badala ya kumzomea Maximo, au kuwachukia wachezaji wanapaswa kuwa wavumilivu. Kwa vile kidole kimoja hakivunji chawa, kocha huyo bado anastahili msaada wa kila mdau wa soka wakati anafanya vitu vyake vya kurejesha heshima ya soka nchini.
Msaada huo si wa kumwambia amchague nani kwenye timu yake wala amfukuze nani bali wa kumjengea mazingira ya kumpatia uwanja mpana wa kuchagua wachezaji wa kuunda timu yake.Kwa muda mrefu klabu za Ligi Kuu zimekuwa zikiambiwa ziwe na timu za vijana. Lakini pamoja na kuelewa umuhimu wa timu hizo, hakuna linalofanyika na Maximo akichanja mbuga mwenyewe kwenda Singida, Songea na Mpwapwa, anaonekana amechagua timu ya ajabu.

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home