“TUUKATAE UFISADI”-DR.SLAA
Jina la Dr.Willibrod Peter Slaa (pichani),Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Karatu, hivi sasa linaweza kuwa jina ambalo linatajwa zaidi kushinda lingine lolote katika anga za kisiasa nchini Tanzania.Wananchi wengi wanamuongelea kama kiongozi shujaa,aliye tayari kudiriki kufanya au kusema chochote katika kutetea maslahi ya wananchi hususani wale wanaoitwa “wa kawaida” na wenye hali duni za kimaisha.Angekuwa anaishi katika nchi za magharibi,Dr.Slaa angeitwa “whistleblower” nambari wani jina ambalo hupewa mtu anayeamua kuwa mkakamavu na kukemea mienendo mibaya na isiyofaa ya watu walioko kwenye madaraka fulani nk, potelea mbali kinachoweza kumtokea kutokana na ujasiri huo.
Kwanini jina la Dr.Wilbrod Slaa liwe vinywani mwa watanzania wengi hivi sasa?Jibu ni rahisi;ni kutokana na mchango wake katika kufichua “ufisadi” uliokuwa unafanyika katika Benki Kuu ya Tanzania(BOT) na mambo mengi mengineyo ambayo anahisi yanakwenda visivyo.
Ingawa umaarufu wa Dr.Slaa haujaanzia na suala la BOT,ni wazi kwamba sakata hili ndilo limefanya jina lake liwe miongoni mwa majina maarufu sio tu kutoka kambi ya upinzani bali katika anga za wanasiasa kote nchini Tanzania.
Lakini Dr.Slaa ni nani?Anatokea wapi?Wangapi wanafahamu alikuwa akifanya nini kabla hajaingia kwenye siasa? Tangu ameingia kwenye siasa amepata mafanikio gani? Anasemaje kuhusu sakata zima la BOT?Ameridhika na maamuzi yaliyochukuliwa na Rais Kikwete?Ana ujumbe gani kwa wananchi?Ili kupata majibu ya maswali hayo na mengineyo, hivi karibuni tulipata fursa ya kufanya naye mahojiano rasmi.Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;
BC: Dr.Slaa karibu sana ndani ya www.bongocelebrity.com. Ni heshima kwetu kupata nafasi hii ya kufanya nawe mahojiano.Jambo la kwanza kabisa ambalo tunaamini wasomaji wetu wangependa kujua ni kuhusu historia yako. Je, unaweza kutueleza ulizaliwa wapi,lini,ukasomea wapi mpaka kufikia hadhi ya udaktari wa falsafa?
WS:Historia fupi, nilizaliwa Kwermusl, Mbulu, Tanzania, tarehe 29.10.1948.Lakini ili kukidhi haja ya swali hili zima,labda tuambatanishe CV au BIODATA yangu kama ifuatavyo;
CURICULUM VITAE(BIODATA)
Full Name: Willibord Peter Slaa.
Date and Place of Birth: 29.10.1948,Kwermusl,Mbulu,Tanzania.
EDUCATION:
PRIMARY: 1958-1961 Kwermusl
1962-1965 Karatu Middle School.
SECONDARY: 1966-1969 Dunguyi Seminary
1970-1971 Itaga Seminary
PHILOSOPHY:
1972-1973 Kibosho Seminary
THEOLOGY:
1974-1977 Kipalapala Seminary
1974-1976 Makerere University,Diploma,Theology
HIGHER EDUCATION:
1979-1981 Pontifical Urba University,Rome,JCD(summa cum laude)
1980-1980 ADV.Diploma-Socio-Political Studies,Koln,Germany(KAF)
1981-1981 St.Thomas Aquinas University,Rome,AD.Diploma Rural Development
1985-1985 London COR.College, Principles and Practice of Management Certificate.
WORK EXPERIENCE:
2000-Todate Member of Parliament(MP),Karatu
1995-2000 Member of Parliament(MP),Karatu.
1991-1995 Executive Director,Tanzania Society for The Blind.
1986-1991 Secretary General,Tanzania Episcopal Conference(TEC)
1982-1986 Development Director,Diocese of Mbulu
1982-1986 Vicar General,Diocese of Mbulu
1977-1979 Development Director,Diocese of Mbulu (Catholic Priest 1977-1991)
MEMBERSHIP IN LOCAL AND INTERNATIONAL BODIES
2006-Todate: Deputy Leader,Official Opposition, Parliament of Tanzania
2000- Todate: Vice President, Forum of African Parliamentarians on Education( FAPED)
2004-Todate: Secretary General,CHADEMA.
2001-Todate: Member,Special Education Committee,MOEC/SADC.
2000-Todate: Shadow Minister,Legal and Constitutional Affairs.
1998-2004 Vice Chairman,CHADEMA
1998-2003 Chairman, Inter-Parliamentary Forum (SADC-PF)
1996-2000 Member,ACP-EU Joint Parliamentary Assembly
1994-Todate: Chairman,Comprehensive Community Based Rehabilitation Tanzania (CCBRT)
1992-1995 Secretart,National Prevention of Blindness Programs,MOH
1992-1995 Director,SLS General Trading Co.Ltd
INTERNATIONAL CONFERENCES
Attended numerous national and international conferences and workshops,presented papers and facilitated in a number of them including,IPU,SADC-PF and CPA organized workshops and conferences.
Attended numerous short courses and seminars both within and outside the country.
BC: Wanasiasa wengi wanasema kwamba waliingia kwenye siasa baada ya kukerwa na mambo fulani fulani wanayokuwa wanahisi hayaendi sawa kijamii,kisiasa au kiuchumi.Kama maelezo hayo yanafanana na historia yako kwenye siasa,ni jambo au mambo gani yalikufanya uingie kwenye siasa?Na tangu umeingia umeweza kuleta mabadiliko gani mpaka hivi sasa?
WS: Niliingia kisisasa mwaka 1995, bila kuwa na nia kabisa ya kuingia kwenye uongozi hasa ubunge japo kwa nafasi mbalimbali nimeshiriki shughuli za Kisiasa huko nyuma. Nimekuwa Katibu wa TANU Youth League nikiwa Kipalapala Seminary, na kufungua matawi mengi ya TANU wakati huo. Nimekuwa Katibu wa Shina la CCM, Tawi la Mambo ya Nje, Rome wakati nasoma Rome, 1980-81.
Niliingia kugombea ubunge baada ya Wazee wa Karatu kunifuata Dar-Es-Salaam, wa vyama vyote vilivyokuwepo wakati ule-CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi. Nikaombwa nichague chama ninachokipenda, na kama ilivyokuwa kwa kila mmoja wakati ule nikaingia kupitia CCM. Nikashinda kwenye Kura za Maoni ndani ya CCM, lakini jina liliondolewa kimizengwe, kwa msingi kuwa “mimi si mwenzao”. Leo ninaelewa kilichomaanishwa, ni kweli kwa hali hii ya ufisadi mimi sikuwa mwenzao”. Sijutii kabisa, kuwa baada ya hapo niliingia Ubunge kupitia Chadema, nafasi pekee iliyokuwa wazi wakati huo. Sikuijua Chadema, sikuwa namfahamu Mzee Mtei, wala Katiba ya Chadema. Nadhani ni Mungu aliongoza hivyo kwa sababu anazofahamu mwenyewe, kwa wale wanaomwamini Mungu.
Jambo kubwa pekee lililokuwa linawakera Wananchi wa Karatu na kuja kuniomba ni : Maji. Karatu ni wilaya isiyo na mto hata mmoja wala maziwa yanayoweza kutumika na binadamu, japo tuna Lake Manyara upande wa Mashariki -Kusini na Lake Eyasi upande wa Magharibi. Wamekuwa wakiomba wapate miradi ya maji kwa miaka 30 lakini licha ya kuchangishwa mara kadhaa miradi hiyo ilishindikana kabisa. Kulikuwa pia na suala la Elimu hasa ya Sekondari na pia matatizo ya Huduma za Afya. Haya ndiyo mambo ya msingi kabisa waliyoomba kwangu wananchi wa Karatu wakitaka niwatangulie na kuwa wako tayari kufanya kazi nami katika hali na mali.
a) Nilipoingia tu, japo sikuwa na diwani, na mwenyekiti mmoja tu wa Kijiji kwa Tiket ya Chadema, na sikuwa na kitongoji hata kimoja, nilifanikiwa kupata msaada mkubwa wa maji kwa ajili ya mji wa Karatu na vijiji vitano vinavyoizunguka vya Ayalabe, Gongali, Gyekurum Arusha, Gyekurum Lambo, na Tloma kupitia shirika la MISEREOR la ujerumani kupitia Diocese of Mbulu, (Katoliki) ambao kwa muda mrefu nimekuwa nikifanya nao kazi na kujenga kuaminiana sana.
Hiki kilikuwa kipindi kigumu sana, kwani mradi huo uliwekewa mizengwe ya kila aina, mbinu za kutaka kuukwamishwa kutumia Katibu Tarafa, Mtendaji wa Kata, watendaji wa Halmashauri.
Hata hivyo, baada ya mapambano makali, kwa kushirikiana na Wananchi na bila Serikali ( ya Wilaya) nilifanikiwa kukamilisha mradi huo mwaka 2000. Siku maji yalipotoka wananchi waliomba dua, walisherehekea, na kuamini kumbe inawezekana. Kuanzia siku hiyo nimeendelea na kutafuta mbinu mbalimbali kupata miradi ya maji kwa ajili ya Wilaya nzima, na hadi leo, vijiji 35 vimepata maji ya uhakika ya Bomba hadi ngazi ya Kitongoji. Kazi iliyobaki ni ya usambazaji hadi karibu na wananchi, kupeleka DP kwa ukaribu wa mita 400 au chini ya hapo kufuatana na sera ya maji ya nchi, na kuingiza maji ndani (Domestic). Pia tumefanya jitihada ya kujenga mabwawa kadhaa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo.
b) Kutokana na maendeleo hayo ambayo yalionekana dhahiri, Wananchi wa Karatu waliichagua Chadema mwaka 2000 na kuifanya CCM kuwa chama cha Upinzani. Yaani Mwenyekiti wa Halmashauri na wenyeviti wa Kamati zote wanatoka Chadema, kutokana na uwingi wa Chadema. Pia katika uchaguzi uliofuata wa Serikali za mitaa 2004, Chadema sasa ina vijiji vingi na vitongoji vingi vinavyoongozwa na Chadema. Wazo hili la CCM kuwa chama cha Upinzani limekuwa gumu sana kueleweka na CCM na serikali yake, hivyo wameendelea kuhujumu Serikali ya mitaa inayoongozwa na Chadema, lakini kwa kuwa tumekuwa imara na tumeendelea kuwa karibuni na wananchi, majaribio hayo yote yameanguka kwenye mwamba wa jiwe.
c) Kwa upande wa Elimu, mwaka 2000 Wilaya ya Karatu ilikuwa na shule moja tu ya wananchi, yaani AWET Sekondari. Lakini kwa Ilani na sera nzuri ya Chadema, tunapoongea leo, Wilaya ya Karatu inayo shule za Sekondari 25, na 3 ziko kwenye hatua ya mbalimbali ya ujenzi. Wakati Sera ya CCM ni shule za Sekondari katika ngazi ya Kata, Sera na Ilani ya Chadema Karatu ni kuwa na Sekondari katika ngazi ya kijiji, kwa vile Kata nyingi bado ni kubwa na shule za kata ni za kutwa hivyo zinakuwa mateso kwa watoto wetu. Zaidi ya nusu ya vijiji tayari vina shule za vijiji za Sekondari. Chadema kwa hili imetoa changamoto kwa Serikali ya CCM. Isitoshe, mwaka huu, 2008 watoto wote wanaotakiwa kuingia Sekondari waliotimiza vigezo, wameingia Sekondari, na bado tuna nafasi tupu 800 yaani tuna madara 20 zaidi kuliko watoto. Kitaifa watoto waliofaulu ni asilimia 51 wakati Karatu waliofaulu ni 54. Tatizo la msingi ni kuwa Serikali kuu inasua sua katika kutekeleza majukumu yake, mathalan upatikanaji wa waalimu ni tatizo kubwa, vifaa vya elimu na hata vitabu.
d) Huduma za Afya nayo ni eneo moja ambapo Chadema tumeonyesha njia. Sera na Ilani ya Chadema ilikuwa kujenga zahanati kila kijiji. Hadi leo ni vijiji 5 tu bado havina zahanati, na vijiji vyote au vimekamilisha ujenzi au viko kwenye hatua ya kumalizia ujenzi. Kutokana na changamoto hiyo, Serikali ya CCM pia sasa imetangaza bila kuwa na sera hiyo ujenzi wa Zahanati katika ngazi ya Kijiji kwa nchi nzima. Tatizo hapa ni Madaktari na manesi ambao ni jukumu la Serikali Kuu na upatikanaji wa uhakika wa madawa.
e) Jambo ambalo mara nyingi linafanyiwa porojo ni kuondoa manyanyaso ambayo wananchi walikuwa wanayapata wakati wa mfumo wa chama kimoja. Chadema Karatu tulipiga vita unyanyasaji wa aina yeyote. Mathalan, michango mingi isiyo ya kisheria inakusanywa kwa mabavu na kuwaumiza wananchi wa chini. Chadema tulipiga marufuku hayo. Ndipo Serikali ya CCM bila kujiandaa ikafuta kabisa kilichoitwa kodi ya Maendeleo. Kwa bahati mbaya walikurupuka bila kuandaa na wala kufanya “alternatives”, na sasa Serikali za mitaa ziko kwenye hali ngumu kujiendesha, na pia kuanzisha dhana mpya ya watu kutolipa kodi ya aina yeyote kabisa.Chadema tulipopiga marufuku kodi za manyanyaso tulitafuta vianzio visivyo na athari kwa mwananchi wa kawaida, wala visivyo na athari kwa uchumi mpana.
f) Miundo mbinu na kilimo ni eneo muhimu ambalo tumeweka mkazo kwa lengo la kupiga vita umaskini kabisa miongoni mwa watu wetu. Mikakati yetu ya kilimo, na jitihada za kutafuta vianzio vyetu vya fedha nje ya vile vya Serikali Kuu imeongeza sana fanaka katika mipango yetu mbalimbali.
BC: Tukiwa hapo hapo kwenye suala la historia yako.Wengi tunatambua kwamba siku za nyuma kabla hujaingia kwenye siasa ulikuwa padre au ulisomea upadre. Unaweza kutueleza kwanini uliacha upadri na kuwa mwanasiasa? Ulifukuzwa au uliacha kwa hiari? Una mke na watoto. Je, kanisa lilikuruhusu kuoa?
WS: Ni kweli nimekuwa Padre wa Kanisa Katoliki. Nimekuwa kiongozi wa ngazi ya juu sana ndani ya Kanisa kuanzia Jimboni kwangu ambapo nimekuwa Makamu wa Askofu, na Mkurugenzi wa Maendeleo, lakini pia nimekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu toka 1985 hadi 1991. Ni kweli hayo maswali yanaulizwa mara nyingi, kwa bahati mbaya si wengi wanaofahamu taratibu za kisheria ndani ya Kanisa Katoliki. Niliondoka mimi mwenyewe katika Upadre bila kushinikizwa na yeyote, wala kufukuzwa, wala hata kupewa onyo. Ni kweli kuna mambo ambayo mimi niliyakataa na kwa dhamira yangu nisingeliweza kuendelea, lakini nadhani hayo ni binafsi zaidi, na si mahali pake kuyaeleza. Nimetoka kwa kibali cha Kanisa, kwa utaratibu wa kisheria wa Kanisa Katoliki, ndiyo maana mimi sina tatizo wala ugomvi wa aina yeyote na Kanisa Katoliki na ninashiriki katika shughuli mbalimbali za Kanisa.
Nina Mke na watoto wawili, Emiliana Slaa na Linus Slaa, japo sijafunga ndoa kikanisa kwa utaratibu wa kawaida wa Kanisa Katoliki, pamoja na kuwa sina kipingamizi chochote kufanya hivyo kikanisa, ni uamuzi wangu na wa mke wangu na familia yetu.
BC: Baada ya mkutano wako wa hadhara pale MwembeYanga jijini Dar-es-salaam Septemba mwaka jana,vyombo vya habari karibuni vyote vilihofia kuandika ulichokisema na pia kuweka bayana orodha ya majina uliyoyataja.Unadhani kwanini vyombo vya habari viliogopa kufanya hivyo? Na wewe binafsi ulijisikia vipi kuona hali hiyo? Tukio lile lilimaanisha nini kwako kuhusiana na suala zima la uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania?
WS: Nilijua kabisa kuwa vyombo vya Habari vinaogopa kuandika aina ya taarifa tuliyotoa na wenzangu pale Mwembe Yanga, hivyo sikushangaa. Nilifurahi sana nilipoona Gazeti dogo la Mwanahalisi, limethubutu, siyo tu kuandika majina na tuliyoeleza bali pia kuweka na picha yao. Tafsiri pekee ni kuwa vyombo vingi vilikosa ujasiri na uzalendo. Vilipenda kujilinda zaidi wasishitakiwe, wengine nao pia hawakuamini tuliyoyasema kama ni kweli na wala hawakwenda mbele zaidi kufanya utafiti wao kuthibitisha tulichosema. Hivyo, kuna mengi yanaweza kusemwa kuhusu vyombo vya habari na uhuru wa vyombo vya habari hapa Tanzania. Hali ni mbaya zaidi, unapokuta kuwa vyombo vingine vinamilikiwa na wanasiasa na hasa pale wamiliki wa vyombo hivyo wanapoguswa kwa namna moja au nyingine na tuhuma hizo.
Waandishi wa habari na vyombo vya habari ni muhimu sana katika ukombozi wa aina yeyote. Wanahitajiwa kuwa na ujasiri, kwani bila hivyo watakosa thubutu ya kwenda kwenye mstari wa mbele wa vita au mapambano kuripoti kinachojiri kama tulivyoona kwa waandishi wa CNN. Nampongeza sana Bwana Kubenea aliyejitosa, na kwa hakika ni shujaa wa kweli, na gazeti hilo dogo limeonyesha njia, naamini na mengine yatafuata njia.
BC: Baadhi ya wananchi,hususani kwenye kambi ya upinzani, wamekuwa wakihofia usalama wa maisha yako.Wengine wamekuwa wakitoa mapendekezo kwamba serikali haina budi kukupa ulinzi wa ziada. Je,wewe mwenyewe unahofia usalama wa maisha yako?Kama jibu ni hapana,kwanini?
WS: Ni kweli hisia hizo zipo na wengi wamenipa ushauri wa aina mbalimbali. Nawashukuru sana kwa kunipenda na kunijali. Hata hivyo, hatima ya yote, Usalama utatolewa tu na Mwenyezi Mungu. Tukumbuke kuwa John Kennedy ameuawa akiwa amezungukwa si tu na maaskari wa ulinzi bali pia na CIA na FBI. Wako waliokufa wamezungukwa na madaktari 30 au zaidi, lakini saa yao ilipofika waliondoka bila kuaga. Ninaacha Maisha yangu kwa Mwenyezi Mungu. Ninachukua tahadhari zote zinazoweza kuchukuliwa na binadamu, lakini kamwe sitaacha kufanya wajibu wangu, na kile ambacho dhamira yangu inataka nikifanye kwa kuhofia usalama na maisha yangu. Hatukuomba kuzaliwa na hatutaomba kuondoka humu duniani.
BC: Watu wengi wamejitokeza hadharani na kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wa kutengua ajira ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu,Daudi Balali.Pamoja na hayo,kumeibuka maswali kadha wa kadha kuhusu maneno kama “utenguzi wa ajira” nk. Tungependa kukuuliza maswali mawili juu ya hili.Kwanza,kwa mtazamo wako,Raisi amefanya kile ambacho ulikitegemea?Pili nini hasa maana ya maneno haya (utenguzi wa ajira) kwa jinsi ulivyoelewa wewe na pia kisheria?
WS: Ni wazi kabisa, msimamo wangu unajulikana na umenukuliwa na magezeti kadhaa:
1) Sijaona kabisa sababu ya kupongeza hatua ya Rais.Kwanza muda uliochukuliwa ni mrefu sana. Jambo hili limejenga matabaka katika nchi yetu. Kwa sheria iliyoko leo, ukituhumiwa unakamatwa, unapelekwa polisi, unawekwa lock up-au unapata mdhamana ambao ni haki yako isipokuwa kwa makosa fulani fulani tu. Lakini kwa tuhuma ya uwizi mkubwa masharti yanajulikana, mathalan kuchukuliwa kwa Passport yako ili usiweze kutoroka, kuweka mdhamana wa mali isiyohamishika kwa kiwango kilichowekwa na sheria nakadhalika, na uchunguzi unafuata baadaye. Hii ndiyo sheria ilivyo leo ( Sheria inayoenda Bungeni inabadilisha kidogo hali hiyo, uchunguzi unatangulia kabla ya kukamatwa). Haya yote hayakufanyika kwa mtuhumiwa wa Mabilioni, tena yaliyothibitishwa na wakaguzi, lakini ameaachwa ana tamalaki tu. Hi si ishara nzuri na wala si utawala bora kutengeneza matabaka kati ya wananchi wake Rais.
2) Hatua ya “kutengua” maana yake Dr.Balali bado ni mfanyikazi wa Serikali, ila tu uteuzi wake au nafasi yake kama Gavana imeondolewa. Wala Rais hajasema kama amesimamishwa kazi au vipi. Angalau basi Balali alitakiwa kusimamishwa kazi Serikalini na wakati Tuhuma zake zinapelekwa mahakamani. Lakini hilo halikufanyika, na kwa msingi huo inawezekana kabisa Balali anaendelea kupokea mshahara kamili, kwa vile hajasimamishwa utumishi wake Serikalini. Isipokuwa kama tutaelezwa vinginevyo, kwa taarifa tuliyonayo Balali ni mtumishi wa Serikali kabla ya kuwa Gavana, na utumishi huo haujasimamishwa.
3) Sijaridhika kabisa na hatua ya Rais, kwa vile, Tuhuma dhidi ya Balali nilizotoa Mwembe Yanga zinaenda zaidi ya Kasma “Vote” moja ya EPA ndani ya BOT.Ziko votes nyingi na ubadhirifu umetapakaa kwingi, kwa mfano fedha zilizolipwa Alex Stewart aliyekuwa anapata 1.9% ya Royalty yetu -ambayo ni 3%. Huu ni mkataba wa ajabu na kama kweli ilifanyika kihalali basi hii ni biashara kichaa kwa maelezo yeyote yale. Suala la malipo kwa Kampuni ya Mwananchi Gold Co halijaelezwa na wala Rais hajalieleza Taifa hatua gani za ziada zinaendelea kuchukuliwa, suala DEEP Green Finance Co halijaelezwa popote ambapo fedha za Umma toka Hazina/BOT zaidi ya 20 Billioni zimepelekwa kusikojulikana, ila kuna ushahidi wa kimazingira kuwa zilipelekwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2005 kuisaidia CCM. Na mengine mengi tuliyoyasema Hizi zote ni fedha za Umma, na Rais hana mamlaka ya kuamua kutoa au kutotoa Taarifa kwa Umma. Ndiyo maana ninaendelea kushinikiza kuwa Tuhuma za Ubadhirifu bado mbichi na hatua zilizochukuliwa hazikidhi kabisa kwa kiwango chochote. Kwa bahati mbaya Watanzania wengi hawaelewi na hivyo wanaridhika tu na kidogo alichokifanya Rais. Tutampongeza Rais atakaposafisha uozo huu wote.
4) Rais alitakiwa kuwasimamisha vile vile wale wote waliohusika na uozo huu. Nimesema mara nyingi kuwa Balali si peke yake katika ubadhirifu na ufisadi huu. Wale wote wanatakiwa kuchukuliwa hatua.Tunaendelea kudai hawa wote wachukuliwe hatua akiwemo Gray Mgonja, ambaye pamoja na yote tuliyosema, anaendelea kuwa Mjumbe wa Bodi ya BOT kwa kofia yake ya kuwa Katibu Mkuu, Hazina. Ni muhimu Rais amwondoe, ili Katibu Mkuu mwingine aingie na kusaidiana na Gavana mpya kusaifisha nyumba. Vinginevyo tunatwanga maji kwenye kinu. Rais ameagiza Bodi ya BOT iwachukulie hatua wahusika wote, ni kweli hafahamu kuwa Gray Mgonja, aliyesaini nyaraka nyingi tu hahusiki kweli, hata kwa uzembe tu? Kama hajui basi tunatatizo kubwa zaidi kuliko tunavyofahamu na tunavyotaka kujiaminisha. Kwa hali hiyo basi ni dhahiri kuwa alilofanya Rais silo nililotegemea wala silo lililotegemewa na Watanzania wengi waelewa wa mambo.
BC: Hivi karibuni umekuwa ukilalamikia suala la serikali kutoiweka hadharani ripoti ya EPA kama ilivyowasilishwa serikalini na kampuni ya Ernst & Young.Unadhani kuna umuhimu gani kwa serikali kuiweka ripoti hiyo hadharani?
WS: Kuweka au kutoweka hadharani kwa Ripoti hiyo siyo hisani ya Rais wala ya Serikali. Jambo lolote lililofanyika kwa Kodi ya Wananchi linapaswa kufikishwa kwa wananchi hasa kama linahusu Tuhuma.
Kwanza serikali yenyewe ilitoa ahadi Bungeni kuwa itawekwa hadharani, kwa wananchi na kwa Wabunge. Itakuwa ajabu kama hata Wabunge hawatapewa. Itakuwa Serikali ya ajabu ambayo haiheshimu ahadi na kauli zake. Waziri Meghji naye pia aliahidi mara nyingi kuwa Taarifa ya Ernst and Young itatolewa hadharani leo kulikoni? Hii hatua ya sasa inazua utata mkubwa, kuna nini kinafichwa?
Pili taarifa hiyo ni muhimu kwa umma wa Watanzania kuona hasa nini kimeandikwa na nani anahusika. Nina sababu nzito ya kuamini kuwa viongozi wa Serikali waliosemwa katika Taarifa hiyo wameachwa nje, na ndiyo maana Serikali inapata kigugumizi katika kuweka Taarifa nzima hadharani. Hili haiisaidii Serikali bali inazidi kuichafua.
Ningependa kuamini Serikali imepata fundisho kwa jinsi ilivyoshughulikia suala hili, na sasa itakuwa makini zaidi, lakini inaelekea wenzetu hawa fundisho bado halijawaingia hata kidogo, na bado wana mawazo ya zamani kuwa Serikali inaweza kufanya inavyotaka. Serikali inayowajibika kwa Wananchi, inapaswa kuwa wazi (Transparent and Accountable). Tuko mbali sana na mambo hayo mawili ambayo ni msingi mkubwa sana wa Good Governance.
BC: Tofauti na hapo zamani,siku hizi taarifa zinasambaa kwa haraka sana.Shukrani kwa maendeleo ya kisayansi na kitekinolojia.Unadhani nini kitatokea katika miaka kumi ijayo kama kasi ya kupeana habari na kuwasiliana itaendelea kukua kwa kasi hii.Wewe binafsi unadhani tekinolojia imekusaidia vipi katika kufanikisha shughuli zako za kisiasa mpaka hivi sasa?
WS: Ni kweli teknolojia imesaidia sana. Hata hili unalofanya wewe ni msingi mkubwa sana katika kupeleka Taarifa kwa watu wengi zaidi. Hili lisingeliwezekana miaka takriban 10 iliyopita. Ninafurahi sana kwa maendeleo haya. Bunge la Tanzania lilipitisha, kupitia Miscellaneous Ammendement sheria kutambua Taarifa zinazopatikana katika Internet, lakini hatimaye Spika wa Bunge akapinga. Nadhani kuna haja kubwa viongozi wetu au kusoma na kupitia maamuzi ya nyuma. Viongozi wengi wanakosa Consistency kwa kusahau waliyoaumua wenyewe, au kupindisha tu sheria makusudi. Kama tunahitaji kwenda mbele ni lazima tuwe jamii yenye principles zisizoyumba na kubadilika badilika kama kinyonga.
BC: Sasa tungependa kukuuliza kuhusu chama cha CHADEMA.Wewe ukiwa kama katibu mkuu wa CHADEMA,unaweza kutueleza chama chenu kina visheni gani kwa taifa? Kama CCM imeshindwa, CHADEMA kinaweza kuwa chama mbadala? Kwa vipi?
WS: Misimao ya Chadema inajulikana wazi katika maswali mbalimbali. Ni dhahiri kuwa CCM imeshindwa kabisa kupiga vita Rushwa, Taifa kwa dhahiri limekosa mwelekeo katika mambo mengi, na CCM na Serikali yake hawataki kusikia, ili kujipongeza tu na miradi kama MMEM na MMES, ambayo kimsingi wala si sera yao ( imetokana na maamuzi ya Kimataifa ya kama vile MMEM na MMES ambayo yalifanyika Jomtien, Thailand, mwaka 1990). Hata hivyo, hatujatekeleza maamuzi hayo kama yalivyokubaliwa yaani EFA. Lakini CCM na Serikali zake kila siku wamekuwa wakijisifu bila kueleza chimbuko halisi la maamuzi hayo. Ndiyo maana hata upatikanaji wa fedha umekuwa rahisi kwa kiasi kikubwa. Mimi nimekuwa Makamu Mwenyekiti wa Afrika wa Wabunge wanaojishughulisha na Elimu, hivyo ninayafahamu kwa undani masuala haya.
BC: Kumekuwepo na habari ambazo zimesambaa mtandaoni zikidai kwamba ndani ya CHADEMA pia kuna kashfa za ufisadi. Shutuma hizo zimekuwa zikielekezwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA na pia wewe mwenyewe.Unasemaje kuhusiana na shutuma hizi?
WS: Ni kweli kumekuwepo na taarifa kama hizo. Siwezi kumjibia Mhe. Mbowe, japo ninamfahamu Mwenyekiti wangu sasa kwa kiasi kikubwa. Na sijawahi kuona wala kushuhudia kinachosemwa. Hata hivyo:
Kwanza kusema au kutoa maoni ni haki ya watu wote. Tofauti ni kuwa hao wanaotoa maoni yao ni ya umbeya, au yanaushahidi kama sisi tunavyofanya? Mimi sina tatizo kama kuna tuhuma dhidi yangu ningelifurahi tu, zitolewe hadharani bila kificho na kwa ushahidi kamili.
Tuhuma zingine zinazoelekezwa Chadema kama za matumizi ya Helicopter, msingi wake tunaufahamu, na tusingelipenda kuwanufaisha watani zetu. Yatosha tu niseme hapa ni kweli, sisi tulikopa fedha kwa Mwenyekiti Mbowe kufanya kampeni zetu. Tuliweka taarifa zetu hadharani. Tukatoa changamoto kwa CCM watoe walipata wapi fedha zao hawajasema hadi leo. Swali la kujieleza, sisi tumekopa kwa Mwenyekiti wetu fedha za Helikopta, na tunamlipa kwa utaratibu uliokubalika kwa mujibu wa taratibu zetu.
Kwa ushahidi uliopo CCM kampeni wamefanya kwa fedha zetu, za Watanzania zilizochotwa BOT, Tangold, Meremeta kupitia DEEP GREEN, sasa nani bora? Nadhani mengine ni propaganda, na watu walidhani hatuna details ya tunayosema. Ninaendelea kui challenge CCM imepata wapi fedha za Kampeni na sources zao zilikuwa nini? Fedha zote zilizochotwa kupitia Deep Green Serikali na CCM lazima wazieleze zilienda wapi? Isitoshe, tulipoanza kutoa tuhuma, ni kwanini CCM walianza kuwakingia kifua watuhumiwa badala ya kuwaacha wajibu wao na au Serikali, lakini Katibu wa CCM anahusika vipi na tuhuma, kama dhamira yake haimsuti kuwa amegunduliwa na ndiyo taharuki ya kujibu hata yasiyomhusu na mwisho kuishia kwenye porojo na propaganda badala ya kujibu hoja?
BC: Ni kiongozi gani duniani anayekuvutia kutoka na jinsi anavyoongoza taifa au jamii yake?Kwanini?
WS: Kwa kuwa sijalifanyia utafiti naomba nisilijibu suali hili.
BC: Tukiachana kidogo na masuala ya siasa,unapokuwa mapumzikoni(tunaamini kwamba hufikia wakati ukahitaji mapumziko)huwa unapendelea kufanya nini?
WS: Nikiwa mapumzikoni mimi hupenda
1) Napenda sana kusoma vitabu mbalimbali vya Sheria, Siasa, maendeleo na hata Novels za kawaida.
2) Kujikumbusha lugha mbalimbali nilizojifunza nikiwa masomoni kama vile Kiitaliano, kijerumani, ili nisije nikazisahau.
3) Kutazama TV.
4) Kufanya shughuli za kawaida na kuzungumza na wapiga kura wangu jimboni.
BC: Mwisho una ujumbe gani kwa watanzania?
WS: Ningependa Watanzania watambue kuwa nchi ni yetu sote. Watanzania katika ujumla wetu ndio wenye nchi, Rasilimali zote za nchi ni zetu sote, na viongozi tumewapa tu dhamana ya kuzilinda kwa niaba yetu. Hivyo, tusiruhusu kabisa wakati sisi tunatumbukia kwenye lindi la umasikini wengine wananufaika kwenye migongo yetu. Kulinda mali zetu, ni jukumu la kila mmoja wetu pale alipo, kwa uwezo alionao na ufahamu wake. Ufisadi uko ngazi zote hadi vijijini tuukatae katakata popote pale. Rushwa tuikatae sote, na Mtanzania hata siku mmoja asikubali kununua haki yake iwe mahakamani, polisi, au hospitalini au popote pale ambapo huduma ni haki yake.
BC: Dr.Slaa,asante sana kwa muda wako.Tunakutakia kila la kheri katika shughuli zako.
WS: Shukrani sana,mimi pia nawatakieni kila la kheri.
1 Comments:
klreoan
Hapo kwa Dr. Slaa umenigusa sana kwani mimi ji mwanaharakati mpigania haki hapa Tz wakina sila ni wenzangu vilevile ni Mwandishi na mtangazaji wa habari katika Radio moja hapa kwetu bongo tuwasiliane nitumie contact zako.
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home