Monday, December 17, 2007

TUNAGHILIBIWA NASI TUMEKUBALI, “TUTAJIJU”

Na: Charles Nkwabi – Tabora

Kisome kisa hiki ni cha kweli wala si cha kuigiza au cha “kubumba”. Jamaa mmoja mfanyabiashara wa ng’ombe kutoka usukumani alisafirisha ng’ombe kupeleka Pugu jijini Dar – es –salaam ili akauze ajipatie “mshiko”. Baada ya kuuza ng’ombe akajitosa jijini na kwa mara ya kwanza akayaona maghorofa marefu ya jiji linalojulikana kama “bongo daresalam”.

Jamaa yule alipoanza kuyashangaa maghorofa marefu akiyakodolea macho, ghafla akajitokeza jamaa mwingine “mtoto wa mjini” akamwambia, “kwa nini unayaangalia sana maghorofa ya serikali? Akaendelea kusema, “Wewe una makosa makubwa, unayakodolea macho majumba yote haya unataka kuyaiba siyo? Hakuishia hapo akaendelea “kukandamiza”, “uko chini ya ulinzi, chuchumaa chini!”.

Jamaa yule ilibidi achuchumae chini kwa kosa la kuyaangalia maghorofa marefu! Inaingia akilini? Baada ya jamaa kuchuchumalishwa akiwa katika hali ya woga na kutetemeka akaulizwa swali “umeyaangalia maghorofa mangapi? Akajibu “matano tu”.
“Haya itakubidi kulipia faini ya kiasi cha shilingi elfu kumi kila ghorofa” yule jamaa kwa kuwa ana “michuzi ana mshiko” wa kutosha, elfu hamsini nini kwake! Akazihesabu haraka haraka “nyekundu za msimbazi” amkabidhi yule jamaa aliyemkamata, ili “mshosha” asije kufunguliwa kesi kubwa mahakamani kwa (kosa la kuyaangalia maghorofa ya serikali kinyume cha sheria)!!

Baada ya kutoa hiyo “fidia” ya elfu hamsini (mtuhumiwa wa kukodolea maghorofa kinyume cha sheria akapewa masharti na yule aliyemkamata kuwa asirudie kuyaangalia maghorofa tena maana kosa kama hilo litamfikisha pabaya!. Mtuhumiwa ikambidi ainge kwenye daladala kurudi nyumba ya kulala wageni alipokuwa amefkia, na alipofika kwa wenzake akajiona yeye ni mjanja sana .

Aliwasimulia jamaa zake masahibu yote yaliyomfika, kisha akasema, “pamoja na kukamatwa mimi ni mjanja sana , hawaniwezi”. Akaendelea kueleza, “nimemdanganya nimeangalia maghorofa matano tu kumbe nimeangalia maghorofa zaidi ya kumi kwa hiyo aliyekuwa amenikamata nimemlipa elfu hamsini tu”! Huku ni kughiribiwa. kujiona mjanja huku unaibiwa mali zako ndio mada kuu ya makala hii.

Mada hii makini iliyonipelekea kuandika makala hii inahusu “kughiribiwa”. Inatia simanzi kubwa mtu anapoibiwa mali zake huku akijivuna kuwa yeye ni mjanja! Inawezekana mtu kama huyu fyuzi za kichwani kwake zikawa zimeunganishwa vibaya ziko (misconnected), anahitaji ukombozi wa kifikra kwanza (open minded on how to perceive things).

Naam, nchi ya Tanzania inazo rasilimali nyingi sana na ina watu wasomi wenye shahada za juu kutoka vyuo vikuu mashuhuri duniani. Rasilimali tulizonazo zinaweza kutosheleza kuendesha bajeti ya nchi bila kuhitaji misaada. Lakini ni dhahiri kwamba tunaghilibiwa na tumekubali na kwa maana hiyo “tutajiju”. Kwa kuukumbatia uwekezaji huku tukikubali kujifunika blanketi ya utandawizi ambao kwa kweli tunaporwa mali za umma badala ya kuzilinda, inashangaza.

Kuna siku nilitembelea shule moja ya msingi huko ughaibuni. Nilipoingia darasani nikainua macho yangu ukutani niliona picha za marais wa Africa wakiwa wameshika vikombe wanaomba misaada. Wanafunzi wakaniambia kuwa marais wengi huwa wakitembelea ughaibuni huwa wanakuja kuomba misaada. Mara nyingi niko kinyume kabisa kwamba sisi watanzania ni maskini. Ni sawa maskini wa nyenzo na teknolojia, lakini ni matajiri sana wa rasilimali. Pengine tatizo kubwa liko kwenye (box) kichwani.

Kwa kupewa sifa kuwa Tanzania tu wakarimu eti “ Tanzania ni kisiwa cha amani”
huku watu wake (walalahoi na waamka vuu) wasijue hatma yao kutokana na kusombwa kwa rasilimali zao mchana kweupe, nao ni ushamba wa aina yake. Pengine tujiulize mali za taifa ni zipi na kivipi zinaporwa na sisi tunaona? Nitaeleza baadae.

Kongamano la wanafunzi wasomi wa nchi hii na viongozi watarajiwa siku za karibuni katika mjadala wao kwenye ukumbi wa DDC Mlimani city, Mwenge jijini Dar – es – salaam moja ya mambo muhimu waliyojadili ni juu ya kuzilinda rasilimali za taifa kwa nguvu zote.

Tujadili na kudai majawabu ya waziwazi juu ya mambo muhimu yanayokwenda ndivyo sivyo mfano suala la Umeme. Wawekezaji waliokuja kuwekeza kwenya umeme wetu wamefanya nini cha maana kama si kuchuma pesa zetu na kuzipeleka makwao?

Uko wapi umeme wa uhakika? Hawa kina Richmond , Ziko wapi zile megawati mia moja ambazo tulikuwa tumehubiriwa kwamba ifikapo mwezi April 2007 umeme utakuwa wa uhakika? Mbona bei ya umeme imepanda maradufu na kusababisha kizazaa na kuyapandisha kasi maisha ya mtanazania? Wawekezaji, wawekezaji, kisa ni kutoka nje ya nchi kumbe ni majizi matupu! Hadi sasa umeme wetu utadhani una ugonjwa wa bonde la ufa sasa umeme huu haukamatiki, kwa wenye umeme unazimika zimika tu tena bila taarifa, kisa mitambo mibovu.

Ni akina nani waliokubaliana na kutiliana sahihi na kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na serikali? Mbona taifa limeuvaa mkenge? Shirika la kimataifa la kupambana na ufisadi – Transparency International (TI) limeripoti mambo ya ukweli kuhusu ufisadi juu ya kampuni ya IPTL. Sasa nani mjanja hapo, ni sisi wabongo au wale tuliongia nao mikataba? Tuna tofauti gani na yule muuza ng’ombe aliyekuwa anayashangaa maghorofa kisha kutozwa pesa?

Mpaka sasa ni watanzania asilimia kumi tu wanaopata umeme, wengine wanaishi gizani. Kuna tarafa kongwe za siku nyingi kama tarafa ya Bukene wilayani Nzega hadi leo hawana umeme. Rais Kikwete alikiri wazi kwenye mkutano mkuu wa nane wa CCM pale Dodoma kuwa, “Athari ya mgao wa umeme kwa uzalishaji viwandani zimesababisha athari ya kupungua kwa bei ya ukuaji wa pato la taifa, upungufu wa chakula, bidhaa za viwandani zikapanda na hivyo kukawa na mfumko wa bei”!

Tuna matatizo makubwa sana Tanzania mojawapo ni siasa za nchi yetu kughubikwa na rushwa ambayo kwa kweli inawagharimu wananchi hasa wanavijiji ambao umeme watakuja kuuona mbinguni kwa Mungu kama watabahatika kufika.

Sula la madini ndio limenza kushughulikiwa baada ya misukosuko mingi. Sekta ya madini inatoa mchango mkubwa katika mapato ya fedha za kigeni. Kwa mujibu wa Rais Kikwete anabainisha kuwa: “madini ni sekta inayokua kwa kasi na inayovutia uwekezaji mkubwa, katika miaka ya hivi Karibuni Tanzania inaongoza Barani Afrika kwa kuvutia kiasi kikubwa cha mitaji” mwisho wa kunukuu. Hii ni sifa kwa Afrika nzima.

Lakini mikataba ya uchimbaji wa madini yetu ina kifafa! Rais Kikwete amebainisha kuwa “kuna kipengele cha kumlinda mwekezaji iwapo atapata hasara kwenye mtaji . yaani iwapo atashindwa kufidia gharama zake za uwekezaji hasara hiyo huhamishwa katika mwaka unaofuatia. Mwekezaji hupewa nafuu ya asilimia 15 ya kufidia hasara hiyo. Maana ya kipengele hicho ni kuwa, mwekezaji atachelewa kuilipa serikali kodi ya mapato na inawezekana asilipe kabisa katika uhai wote wa mgodi”.

“Kipengele hicho kililenga kumlinda mwekezaji asipate hasara, ikasahau kumlinda Mtanzania anayepata hasara ya madini yake yanayochukuliwa kwa ajili ya kufidiwa hasara anayopata mwekezaji”, anatanabaisha Rais Kikwete.

Rais Kikwete ameeleza wazi kuwa tayari “ Nikalipigia kelele jambo hili tena katika majukwaa ya kimataifa, nikataka tuzungumze, bahati nzuri wakasikia, tukazungumza na baadhi ya kampuni tumeelewana, baadhi bado tunazungumza. Hivyo, kipengele hicho kiondolewe tubaki na mfumo wa msingi uliopo kwenye sheria ya madini. Kwa ajili hiyo makampuni kadhaa yataanza kulipa kodi muda si mrefu”.

Najiuliza maswali ni kina nani walioliingiza taifa kwenye mkenge wa namna hii? Tulikuwa wapi kuyalinda madini yetu tangu mwanzo? Hatukuwa na uchungu na rasilimali hii adimu kwa mataifa mengine? Hebu nenda leo hii Uarabuni ambako rasilimali yao ni mafuta, inawafaidia wazawa wa nchi husika. Barabara zao ni za mkeka na hawana shida ya maji hata kama wanaishi jangwani! Ni Tanzania pekee ndio tunaoghiribiwa. Awamu iliyopita ndio inapaswa itoe majawabu ya maswali haya.

Ndio, ni Tanzania pekee inayoghiribiwa kwa danganya toto jinga, kudanganyiwa misaada huku tunaibiwa vyetu. Nenda Ghana wawekezaji kwenye sekta ya migodi wanalipia asilimia 50 ya pato la madini. Botswana wawekezaji wanalipia asilimia 37 ya mapato katika sekta ya madini pekee mbali na malipo mengine kama vile technical services, management fees nk.

Kuporwa kwa mali ni janga zaidi ya janga la Ukimwi. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kikwete amekuwa akiongoza mapambano dhidi ya Ukimwi kwa nguvu kubwa sana . Homa ya bonde la ufa ilipigwa vita sana mpaka imetokomezwa. Sasa Rais wetu Kikwete ulishapewa rungu la urais, liinue ikiwezekana lipige mtu mmoja (yaani afukuzwe mtu kazi na kushtakiwa) ahojiwe kwa nini alipora rasilimali za taifa? Kwa nini tushtuke baada ya miaka kadhaa. Na tunapokuja kushtuka ndipo tunakuja kuunda kamati! Kama huna rasilimali zako mwenyewe huchukui muda utakuwa mtumwa wa wenye nazo!

Kwa bahati mbaya tulishaachwa yatima na baba yetu aliyekuwa na uchungu wa kuilinda rasilimali za nchi kwa faida ya vizazi vijavyo, Baba wa taifa atakumbukwa milele yote, alikuwa ni muonaji anayejali maskini, alijali sana utu wa mtu badala ya kukumbatia mautanda –wizi kama yaliyopo leo.

Zamani enzi za uhai wake Mwalimu Nyerere alikuwa amekataa kwamba sio kila sekta lazima iuzwe. Leo hii uchumi wa Tanzania umo mikononi mwa wageni na si wazalendo kwani njia kuu za uchumi “zimetekwa” kama vile madini yetu, mafuta, viwanda vyetu ambavyo vingi vimenunuliwa na waasia au wazungu..

Waangalie wakulima wetu leo hii utawahurumia. Wanalima tumbaku na wanalipwa bei ya kutupwa huku wakiwa wamekopeshwa mbolea kwa bei ya kuruka sana , nani awasemelee, kila atakayesema ataonekana ana njaa…Wakulima hawa kila wanapouza mazao ya tumabu wanaambulia kiduchu, sababu hakuna wa kuwasimamia katika mauzo yao . Kampuni la ATTT inawakamua tu. Mamlaka za za kiserikali hazina ubavu kwenye makampuni haya.. Kwa nini vyama vya Ushirika viko wapi na vinafanya nini? Tnaghiribiwa na tumekubali, tutajiju.

Mbunge wa Nzega CCM Mh. Lucas Seleli ni “mwanaume”, alifoka bungeni akihoji kwa nini mbolea imegeuzwa kuwa ni biashara ya kulangua kwa wananchi? Akahoji kwa nini wakulima hawasaidiwi kupata mbolea kwa bei nafuu..

REDET, taasisi ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar –es – salaam ilisema juzijuzi kuwa wananchi wengi wameridhishwa na utendaji wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete nami nampa bravo, much congratulation my president! lakini wananchi hawaridhishwi na utedaji wa mawaziri! Lazima majawabu yatafutwe haraka ili kuifanya Tanzania iwe na dira sahihi ya kimaendeleo. Kujuana kwenye masuala ya kazi huwa kunaumiza shirika ama kampuni.

Sheria za kazi, uwajibikaji ukiwepo, heshima baina ya mtu na mtu na baina ya mtu na rasilimali za taifa italiendeleza taifa letu na kuwafikisha Kanaani watanzania. Kiongozi anatakiwa awe anaaminika kwa watu, kwa serikali na kwa chama chake. Kiongozi anapaswa kuwa mwadilifu katika utendaji wake wa kazi yake. Profesa John Eduku Adoku wa Chuo Kikuu cha Makerere jijini Kampala siku moja alituuliza swali ambalo halikuwa na majibu, labda wewe msomaji unajibu, alisema: “where are the leaders of integrity in Africa ”, akimaanisha wako wapi vingozi wenye uadilifu barani Afrika? Tujadili.

E – mail: nkwabicharles@yahoo.co.uk Simu: 0754 555680

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home