Monday, December 17, 2007

TANZANIA NI “KISIWA CHA AMANI” KINACHOZALISHA MAOVU NA KUIKIMBIZA AMANI

Na: Charles Nkwabi – Tabora

Miaka 46 ya uhuru wa Tanganyika , Tanzania kwa leo ni kipindi kirefu, ni umri wa mtu mzima. Je kuna cha kusherehekea? Ndio, tuna haja ya kujivuna na kusherehekea. Bravo kwa kila Mtanzania. Lakini kwa nini tusherehekee na nini cha kujivunia ama mafanikio gani tumeyapata mpaka “tuselebuke” yaani tufurahi juu ya Uhuru wa nchi hii? Majibu yako mengi sana . Pamoja na majibu mazuri, kuna kitu kimeibuka ambacho kinatia kichefuchefu kwa uhuru wetu.

“Tuna maana gani tunapoongelea uhuru? “… kuna uhuru wa mtu binafsi, yaani haki yake ya kuishi kwa hadhi na usawa miongoni mwa watu wengine, haki au uhuru wake wa kuongea, uhuru wa kushiriki katika kufanya maamuzi yote yanayohusu maisha yake…” mwisho wa kumnukuu mwasisi wa taifa letu, Mwalimu J. K. Nyerere.

Kama hujui ulikotoka na ulipo, uendako hufiki. Tanzania ya leo inasifika sana hapa duniani kwa sababu nyingi tu. Mosi Tanzania hadi leo hii ni “kisiwa cha amani”. Kwamba hatupigani vita hata kama kuna makabila 125 na bado tunawasiliana kwa lugha moja ya Kiswahili. Jambo hili linawakoga sana watu wa jumuia ya kimataifa.

Nilikuwa ughaibuni nchi za Ulaya, Ukisema unatoka Tanzania unapata picha halisi kwamba wenzetu wanatuonaje. “ Ooh unatoka Tanzania nchi ya Nyerere”. Nami nikajibu “naam”. Kumbe wakati huu Tanzania imepaa katika kujulikana kwake kuanzia London , Stockhom, Helsinki , Oslo hadi Paris .

Pili, Tanzania inasifika kutokana na mchango wake mkubwa wa kuzikomboa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara . Nchi karibu zote za kusini mwa Afrika zilipata ukombozi wake kutoka Tanzania , ambapo mipango ya utekelezaji juu ya ukombozi ilikuwa ikifanyika jijini Dar –es – salaam. Shime itengenezeni Dar – es – salaam iwe safi kimazingira na vurugu za daladala zimalizwe haraka. Jiji la Dar liwe “bomba”.

Balozi mstaafu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mh. Daudi Mwakawago anasema ni lazima tujivunie “Amani yetu” na mafanikio makubwa ambayo yamepatikana. Tumefikia mafanikio makubwa sana tangu tupate uhuru na tuna haki ya kusherehekea. Tunajivunia amani yetu. Sasa ni miaka 46 ya uhuru wa Tanganyika , naam yanaonekana kuwa safi upande mmoja wa shilingi.

Takwiimu zinatuonyesha wazi lazima tusherehekee. Tumekuwa na uwezo wa kujisimamia mambo yetu wenyewe bila wakoloni. Watu waliozaliwa baada ya mwaka 1961 hawajui sana juu ya kwa nini tusherehekee. Watanzania kwa sasa ni watu huru katika nchi huru.

Tanzania kwa sasa ina jeshi lenye heshima kubwa kwa mfano JWTZ tumeshuhudia wanajeshi wetu wakienda kwenye mataifa mengine kwa ajili ya kulinda usalama kama vile Liberia , Sudan na kweingineko. Pia tunalo jeshi la JKT nalo liko imara sana pamoja na jeshi la Polisi na lile la Magereza. Jamaa mmoja alitolewa nyoka pangoni kutokana na ushenzi wake wa kuivamia Tanzania huru naye si mwingine ni Idd Amin aliyeivamia Tanzania miaka ya sabini na akaishia kusikojulikana, Kwa nini tusiwe na furaha kwa kuwa tu huru?

Kielimu kumekuwepo mapinduzi makubwa katika sekta hiyo. Mipango ya MMEM na MMES imeleta mageuzi makubwa kama vile shule zilizokuwa zinaonekana kama magofu sasa zinang’aa hadi vijijini. “Tukifanya tathmini ukilinganisha na kule tunakotoka leo hii elimu imekuwa bora na inaendeleza watu kupitia programu za MEMKWA ambapo idadi ya wanaojua kusoma na kuandika sasa imepanda. Pia elimu ya leo imeweza kuendeleza rasilimali watu (human resource) nk..” Anasema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar – es – salaam Dr. Azavael Lwaitama.

Kuna mengi ya kujivunia kama vile baadhi ya barabara sasa zinapitika hata wakati wa masika. Sekta ya afya nayo inajitahidi kusogeza huduma kwa wanajiji. Kinachotia ukakasi ni kilimo. Kilimo chetu kinakwenda kwa kuchechemea. Kinachotia kichefuchefu ni suala zima la uchumi. Ni mbaya sana kuua viwanda. Viwanda vyetu ndio kwanza tumeviua kabisa katika kipindi hiki cha uhuru wetu. Suala hili linahitaji mjadala mpana sana na utekelezaji wa haraka, vinginevyo tumekwisha.

Zamani hakukuwa kuna kuhoji viongozi. Watu wengi walikuwa woga wa kuhoji lakini leo hii watu wasiojua kusoma na kuondika hata wao wana ujasiri wa kuuliza na kuhoji. Watu wanahoji bwana, wanataka wajue mustakabali wa maisha yao . Kama Mungu alihojiwa na akabadlisha sera zake za kuwaangamiza wenye haki pamoja na waovu, sembuse binadamu (just a mere human being)? Wakitaka waende mahakamani waende, lakini kuhoji sio dhambi, mtu akikosea lazima aonywe hata awe nani..

Bila elimu hakuna maendeleo. Pamoja na programu nzuri na kubwa juu ya elimu bado kuna mfumo wa elimu unapaswa uangaliwe upya na urekebishwe. Ni lazima tujiulize Je mfumo wetu wa elimu ya leo hii una matatizo gani? Elimu ni ya nini siku hizi kama wanaosoma hawasaidii kubadilisha maisha yetu, kama wanaosoma wanasoma na kupata shahada lakini bado mali za taifa hili zikiporwa tu .. elimu ya nini basi?

Waziri mstaafu na Balozi wa Umoja wa Mataifa wa Tanzania Mh. Daudi Mwakawago juzijuzi amesema “ni lazima tufikiri tunawapa elimu gani wanafunzi wetu. Tunawapa vyeti ama taaluma”. Taaluma wanayoipata inawasaidiaje? Jibu ni rahisi Wengine wanajiajiri na wachache wao wanaajiriwa. Unaweza kuwa na wasomi wataalamu lakini sera zako zikoje, na mazingira ya ajira yakoje ndio mambo muhimu ya kuhoji…

Mfumo mzima wa elimu yetu hapa Tanzania haumwandai kijana baada kumaliza shule kidato cha nne au cha sita afanye nini baadae. Ni elimu hii ambayo tumeirithi kutoka kwa wakoloni, elimu ambayo haina wala haitambui mazingira ya Tanzania . Tanzania tumeweka sana uzito kwa kufaulisha wanafunzi na mtu akishapata kazi basi hajishughulishi tena na kujisomea vitabu ili akili yake iwe fresh kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Myerere, Mwasisi wa Uhuru wa nchi hii. What I can say, “Our education is so better but we need to translate it into the implementation..” hii ina maana elimu yetu ni lazima tuitafsiri katika utekelezaji.

Mfumo wetu wa elimu Tanzania ya leo ni wa kuzugana. Mwenye nacho hapeleki watoto wake kwenye shule za “yeboyebo” shule za kata za “kina -Kayumba”. Kwenye shule hizo hazina vitabu wala maabara naam hata waalimu wake ni wa “vodafasta” maana wamepewa mafunzo ya ualimu kwa mwezi mmoja tu hata kama hajajifunza somo la Psychology twende tu, mtu anakuwa mwalimu mkuu, huu ndio uhuru wetu wa miaka 46.

Leo hii kuna idadi kubwa sana ya watoto wanaoingia shule za msingi na Sekondari, lakini halijapatikana jawabu kwamba wakimaliza kusoma watafanya nini kwa sababu sera ya ajira na mazingira yaliyopo yanakataa kabisa kumwajiri mtu anayemaliza shule moja kwa moja isipokuwa kazi ya ualimu haina mizengwe maana huwa hakuna masharti ya uzoefu wa kazi (experience of work) wa miaka mitatu na kuendelea..

Tunaposema kwamba Tanzaia tuna amani ni lazima tuipime kwa undani zaidi. Amani hiyo isitumike vibaya kuwakandamiza wengine huku viongozi wahusika wakijinufaisha. Amani ya Tanzania ina maana gani, ni maeneo gani ambayo kuna amani. Tusiseme amani tu tukimaanisha hakuna vita.

Leo hii kuna mizengwe kibao kwa vijana wanaotafuta kazi ama ajira hata kama ni wataalamu na wamemaliza shule na wana vyeti vyao vizuri. Kama huna refa wa kukusemelea, kukutafutia mwanya wa kufanya kazi utasota sana . Kwa upande wa wasichana wao huombwa rushwa ya ngono ndipo waajiiriwe na hakuna cha interview! Je kuna amani hapo? Kama mtu bosi fulani alisoma kwa shida shuleni na ndio kinakuwa kigezo cha kuwakomoa wengine. Je hapo hatuzalishi maovu kwa wale watakaofuatia katika taasisi zetu?

Kwa nini hali yetu inazidi kuwa mbaya mbaya zaidi katika maeneo ya ajira, kichumi nk? Elimu bora ni ipi na je elimu yetu ina mchango gani katika kuujenga uchumi wetu? Wanafunzi wa nchi hii baada ya uhuru wanafaulu sana . Haya ni mafanikio. Swali, leo hii vijana wetu wanapomaliza shule na wasipate ajira waende wapi? Tunataka wawe wamachinga au mama lishe siyo?

Mwasisi wa Uhuru wa nchi hii Mwalimu Julias Kambarage Nyerere enzi za uhai wake alisisitiza akisema nami namnukuu: “… elimu inatakiwa kuwaandaa vijana wetu kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa… ambamo mabadiliko ya maendeleo yanapimwa kwa kuzingatia ubora wa maisha ya mtu na siyo majengo ya kifahari, magari, au vitu vingine vya aina hiyo”. Mwisho wa kunukuu.

Kukosekana kwa somo la “Maadili” mashuleni kumewafanya vijana wetu wasijue wala kuona umuhimu wa haki za binadamu. Somo la maadili ni pana sana , linahusu kuthamini utu wa mtu, heshima, uzalendo pamoja na kuendeleza rasilamali zako na si kuzihujumu. Somo la Maadili linagusa uadilifu, uwajibikaji na uwazi. Somo la Maadili lingefundishwa shuleni kuanzia shule za Msingi, Sekondari hadi vyuo vikuu adabu ingekuwepo.

Vijana wetu wangejua kuwa kumfanyia mtu mwingine vitendo vya aibu na vya kinyama kama vile kuomba rushwa ya ngono, kumyima mtu ajira ni dhambi ambayo haina msamaha hata kwa Mungu. Leo hii tunapoona vitendo vya rushwa, “ufisadi” ni matokeo mabaya ya watu kunyimwa haki zao. Rushwa na ufisadi inachochea sana kuvunjika kwa amani tuliyonayo.

Misingi aliyoiacha Baba wa taifa hili Mwalimu Nyerere sasa inaonekana si lolote si chochote! Mwalimu Nyerere aliicha misingi mizuri sana . Mwalimu Nyerere licha ya kuwatetea wanyonge na kukataa urafiki na wabakaji wa uchumi wetu pia aliweka msingi wa kuwandaa viongozi bora.

Enzi za uhai wake Mwalimu Nyerere kulikuwa kuna vyuo tisa vinayotoa mafunzo ya uongozi. Hadi leo tukisherehekea miaka 46 ya uhuru hakuna hata chuo kimoja kilichosalia cha kuwandaa viongozi wa nchi hii. Kukosekana kwa vyuo vya kuwandaa viongozi kuna athari kubwa sana , tutajadili kwenye matoleo ya gazeti hili hapo baadae.

Ndio maana watu leo hii wanatumia amani kama kigezo cha kujinufaisha wenyewe. Mwalimu Nyerere leo hii kama angefufuka angechukua fimbo na kuwachapa wale wote walioigezuza nchi hii kuifanya biashara kwa mikataba mibovu iliyopelekea kuundwa kwa kamati mbalimbali kuchunguza ubedhuli uliokwisha kufanyika.

Ikumbukwe kwamba Bwana Yesu alipoona nyumba ya kuabudia imegeuzwa matumizi yake aliwachapa fimbo wote waliokuwemo ndani ya nyumba akazipindua meza zao akisema “kwa nini mmeigeuza nyumba ya Baba yangu, nyumba ya sala kuwa pango la wanyang’anyi”. Mwalimu Nyerere angefufuka leo angesema “kwa nini Tanzania mmeigeuza na kuiuza kwa wageni kwa sera mbovu za ubinafsishaji na utandawizi huku mkiwaacha wenye nchi wakihangaika kwa kukosa viwanda vyao wenyewe? Angalia leo hii watanzania walio wengi wana mawazo ya kiumaskini, wanakula wasichozalisha na wanazalisha wasichokula. Kwenye maduka ya wabongo hakuna bidhaa zao wenyewe.

Tuna machungwa, tuna maembe lakini yanajiozea tu hapa Tanzania . Hatuna viwanda vya kutengeneza juice hata kama kule Muheza, Lushoto mpaka Tabora kuna matunda kibao lakini tunakunywa jice za Afrika kusini na za Uingerza!. Kule Manispaa ya Tabora maembe sasa hayazai kabisa kutokana na miti mingi ya maembe kukatwa matawi kwa shoka ili watu wapate kuni za kuchomea matofali!


Mgawanyiko wa matabaka yaliyopo leo nchini Tanzania ndio issue inayoondosha amani nchi hii. Mwalimu Nyerere akitokeza tu “tit for tat” ama kwa vubu vaba” yaani ghafla bin vu, atawatimua baadhi ya watendaji wabovu wa nchi hii. Sasa hayupo tena nani akemee…

E – mail:
nkabicharles@yahoo.co.uk Simu: 0754 555680

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home