Monday, December 17, 2007

UKIMWI UNAPIGIWA NGOMA, DISCO NA COMEDY WATU WANAHAMASIKA KUPIMA

Na: Charles Nkwabi – Tabora

Rais Jakaya Kikwete alishapima na mkewe Salma Kikwete wakaonyesha mfano ambao wengine wanapaswa kufuata nyayo za viongozi wao. Ukiwa huna virusi waweza kujisikia salama zaidi na unakuwa mwangalifu zaidi. Hivi kupima kunasaidia nini?

Kabla Rais hajafika mjini Tabora na kuhitimisha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo huazimishwa December mosi, mkoani Tabora mwamko wa kupima VVU kwa hiari ulikuwa mdogo sana mpaka vikundi vya ngoma, disco na Comedy viliposhuka dimbani ndani ya uwanja wa Chipukizi, kukawa “kumekucha”.

Kumbe watu wanapenda sana burudani kuliko kitu kingine! Shime safu hii ilijionea watu kutokujitokeza kupima kwa hiari karibu wiki mbili kabla ya “kumwagika” kwa vikundi vya burudani vikiwemo vya kina mzee Small kutoka Dar –es –salaam. Kwaya mbalimbali zimekuwa zikiimba nyimbo zenye tija juu ya Ukimwi.

Kumbe ili ufanikishe mambo yako kwa jamii ukiwatengea ngoma kama vile Sensema Malunde, bendi maarufu mkoani Tabora utawapata watu kibao naam utafanikisha lile unalolitaka!

Sitoki nje ya mada, mada yangu ni suala la Ukimwi. Ukimwi si suala geni masikioni mwa watanzania walio wengi mpaka vijijini. Angalau kila familia imewahi kuguswa na gonjwa hili ambalo linawapukutisha watanzania na linatia simanzi kwa familia, likipunguza kwa kasi mpya wataalam wengi na rasilimali watu (human resource) hadi serikali inapata hasara kubwa sana .

Imepigwa mbiu ya mgambo kwamba “ Tanzania bila Ukimwi inawezekana”. Hapa ndipo kwenye kiini cha makala hii ambayo kutokana na ufinyu wa nafasi gazetini nitagusia mambo machache tu.

Ili kweli Tanzania iweze kutokuwa na Ukimwi mipango inayokwenda sambamba na vitendo ifanyike kwa kumaanisha yaani (seriously). Kamwe ugonjwa huu hatari usigeuzwe na kuwa “dili” la kujinufaisha kwa baadhi ya watendaji wa serikali, wakurugenzi wa asasi na hata wafadhili wanaotoa misaada ya fedha kusaidia makabwela na makapuku barani Afrika.

Ukimwi usifanywe kuwa ni kitu cha kuchezea, la sivyo Tanzania ibakia “mahame” au pango la wanyang’anyi. Kwani hatujui kuwa ni asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijijini? Huko vijijini watu wanapatiwa elimu ya Ukimwi ya kutosheleza? Ni kiongozi gani ama asasi ipi kusema na ule ukweli inawahudunia wanavijiji?
Itawezekanaje Tanzania bila Ukimwi kama wanavijiji wamesahaulika na hakuna anayewajali kuwapelekea elimu sahihi ya Ukimwi na hata kuwahudumia wale ambao tayari wamekwisha kuathirika?

Thamani ya mtu inapimwa kwa kipimo kipi kama baadhi ya watu walifikia hatua ya kueneza virusi vya Ukimwi duniani? Ni Muumba wetu pekee ajuae thamani halisi ya binadamu. Mara nyingi sisi wanadamu tunadanganyana tu. Mtu akipatwa na VVU si kwamba ndio mwisho wa maisha yake. Anaweza kuendelea KUISHI kama kawaida asiponyanyaliwa na wanafamilia, ndugu au kazini kwake.

Tanzania bila ukimiwi itawezekana vipi kama utu umetutoroka? Mabosi wengine wamekuwa na tabia za fisi! Mabosi wanaotaka rushwa ya ngono ndio watoe ajira!. Bosi yeyote kama hutaki kuajiri usiwasumbue wenzako. Hii rushwa ya ngono inaendeleza Ukimwi.

Tanzania bila Ukimwi itawezekana vipi kama ustaarabu umetutoka? Watu wazima na ndevu zao kufuata – fuata vitoto vya shule na kuvitongoza? Je hamjui kuwa ngono ndio namba moja ya maambukuzi ya VVU? Watu wazima wanavifuata visichana vidogo kwa kuwa vingi havina VVU! Kwa mtindo huo Tanzania itabaki bila Ukimwi?

Tanzania bila Ukimwi itawezekana vipi kama tunadai kuwa bajeti haitoshi kuwafikia wanavijiji? Kwani bajeti ya fedha na uhai wa mtu kipi zaidi? Inashangaza sana tunadai kwamba elimu ya Ukimwi iwafikie wanajamii wote huku waandishi wa habari hakuna anayewafikiria kuwapa mafunzo ya kuipeleka elimu ya Ukimwi kwa jamii!

Tanzania bila Ukimwi itawezekana vipi kama watu hawajahamasika vya kutosha kujikinga na ugonjwa huu hatari? Je suluhisho la Ukimwi ni kupima tu? Sawa kupima ni moja ya faida ya kupambana na Ukimwi kwani faida ya kupima ni kufanya maamuzi sahihi baada mtu kupima na Kikwete alishaonyesha mfano..

Tanzania bila Ukimwi itawezekanaje kama watu ama mtu mmoja mmoja hajabadili tabia ya kihuni? Kama mtu anakunywa pombne na kulewa anawezaje kujitawala mwili wake? Kama mabinti wetu wanavaa vivazi vinavyoacha wazi viungo nyeti vya uzazi na kwenda disco ukimwi utapungua kweli? Kama hakuna heshima ya utu wa mtu tutaweza kuwa Tanzania bila Ukimwi?

Umaskini wa vipato kwa familia nyingi ni suala zito sana nchini Tanzania . Swali kama wanawake ama wasichana hawana vipato vya kujikimu kimaisha itawezekana kujiepusha na vitendo vya ngono ili wapewe pesa na hivyo kuifanya Tanzania bila ukimwi kuwezekana?

Ni asasi gani inawapa uwezo wanawake wa vijijini wasiokuwa na waume kuwajengea uwezo wa kuwa wajasiliamali ili wajitegemee kimaisha na wasifanye ngono holela? Hoja ni nyingi nafasi haitoshi.
Kuwawezesha wanawake kujitegemea kiuchumi na kutoa elimu sahihi ya Ukimwi kwa kila mtu ni ufumbuzi sahihi wa Tanzania bila Ukimwi kuwezekana. Lakini kupima pekee si suluhisho la Tanzania bila Ukimwi kuwezekana. Tuchukue hatua zaidi ya hapo

nkwabicharles@yahoo.co.uk simu: 0754 555680

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home