Monday, December 17, 2007

HATIMAE UKIMWI UTAGEUKA KUWA HISTORIA, TUKAZE MWENDO – BALOZI, MH. MARK GREEN

Na: Charles Nkwabi – Tabora

“Sisi sote tunaioshi katika nyakati zenye misukosuko, tunapitia nyakati za kihistoria. Kama kuna nyakati za maji kujaa na kupwa katika matukio ya maisha ya binadamu, basi ni dhahiri kuwa hivi sasa tuko katika kipindi ambacho historia inaandikwa kwa mwendo kasi sana ”. Anasema Balozi wa Marekani nchini Mh. Mark Green kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo kitaifa yalifanyika mjini Tabora December mosi.

Mh. Mark Green anasema “Katika miaka ijayo, ninaamini tutakuja kutazama na kuziona nyakati hizi kama wakati muhimu katika historia ya binadamu. Katika nyakati hizo zijazo, watoto wetu na wajukuu wetu watapenda kujua ni kitu gani alichokifanya kila mmoja wetu katika vita dhidi ya Ukimwi, tulikuwa upande wa nani, tulijitoa kiasi gani”.

“Tulifanya nini kila mmoja wetu dhidi ya Ukimwi na tulijitoa kiasi gani” ndio kiini cha makala hii na ndicho kilichonisukuma kuandika makala hii kwani baadhi ya watu wanaona Ukimwi ni “dili” la kujipatia mali na kujipatia ajira ya kudumu!

Ukimwi ni gonjwa la dharura, tunahitaji kuwa na mitizamo anuwai ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi. Mh. Mark Green anabainisha kuwa “sisi kama jumuia ya kimataifa, tukifanya kazi kwa ushirikiano, hatuna budi kuungana pamoja kuwasaidia wananchi – kwa kushughulikia mahitaji kwenye ngazi ya huduma, na papo hapo kuimarisha mifumo ya afya kitaifa.”.

Kwa kuwa Ukimwi ni ugonjwa wa daharura, kumbe hii ni vita bab kubwa! Mataifa tajiri yanasema “kupitia mikakati yetu ya kutoa misaada kwa pamoja kama (Donor Partner Group on HIV and AIDS), tunaweza kufanya kazi kuwahudumia wale ambao wanahitaji msaada wetu leo. Na pia kujenga mifumo ya huduma za afya nchini Tanzania , na ambayo inaweza kutubeba kuingia katika nyakati zijazo, na kunasa kihalisi uwezekano wa kufanikisha mikakati ya kuwa na Tanzania isiyo na Ukimwi”

Balozi Mark Green anafurahishwa na mapambano ya Ukimwi, akielezea anasema, “Nimeona kupitia mikakati mbalimbali ya wahisani kutoa ufadhili, jinsi Tanzania inavyoweza kukabiliana na Ukimwi katika kipindi cha sasa hivi na kipindi cha muda mrefu. Ushirikiano wa kimataifa umeleta mabadiliko halis, sio tu katika ngazi ya kidemokrasia, bali pia aktika maisha ya kila siku kwa watu wanaoishi maisha ya dhiki nchini kote”.

Katika mapambano juu ya janga la Ukimwi Balozi Mark Green anamwelezea Rais Kikwete kuwa: “Mikakati ya jumuia ya kimataifa katika kupambana na UKIMWI iko dhahiri, kwamba imetiwa nguvu na kauli ya Rais Kikwete, “ Tanzania bila Ukimwi inawezekana”. Uongozi wa Rais Kikwete unapata mafanikio nchini kote Tanzania , na maneno yake (Rais Kikwete) yanasikika kimataifa. Mh. Rais, wewe na Mama Kikwete ni mfano bora kwa wanandoa wanaokwenda kupata ushauri nasaha na kupima”.

Mh. Rais, uongozi wako na juhudi zako za dhati kuboresha afya ya wananchi wa Tanzania imewapa ujasiri Watanzania wasio na idadi kutafuta taarifa kuhusu afya zao, amabzo zitabadilisha maisha yao . Uongozi thabiti, ulioonyeshwa na Rais, ni muhimu kama tunataka kuutokomeza ugonjwa huu na kufanikiwa kuzuia kuenena kwa UKIMWI”.

Kama viongozi wa Tanzania , kila mmoja wenu anaandaa njia ya kufanikisha kuwepo kwa taifa lisilo na UKIMWI… kwa mujibu wa maono ya Rais Kikwete, Tanznaia bila Ukimwi inawezekana.

Mh. Mark Green anasema, “Tunapaswa kuongeza juhudi zetu maradufu kama tunataka kufanikisha maono ya Rais Kikwete, na siyo tu kuyaacha yakabaki kuwa matumaini au ndoto”.

Imezuka tabia kwa baadhi ya watu katika kupambana na vita hii ya Ukimwi kwao imekuwa ni “dili”, Mh. Mark Gree anaonya, “Hakuna kitu kibaya zaidi kwa maelfu ya wananchi wanaoishi… na walioathirika na Ukimwi kama vitendo vibaya vya watu wachache vinavyoambatana na kutokuwajibika. Wote hatuna budi kufanya kazi kwa pamoja kuimarisha juhudi za kupiga vita rushwa. Juhudi za mapambano ya vita ya Ukimwi iwe endelevu”.

Changamoto ziko nyingi juu ya Ukimwi, mosi matumizi ya fedha zinazotoka kwa wafadhili kama vile Global fund, Marekani , Japan na kwingineko zitawafikia wananchi wa vijiji vya Itanana, Ifucha na Itobela mpaka Kahama ya Nhalanga huko Tabora? Suala la Ukimwi ni la kuhusu kuokoa maisha ya watu na si kutumia mapesa yaliyotengwa kuhudumia watu unaamua kununua magari ya kifahari yenye vioo vya giza !

Shime wale wote wanaoendesha vitendo vya kinyama juu ya suala hili nyeti la Ukimwi, umefika wakati fagio la chuma la Jakaya Kikwete lianze kuwafagia, wamulikwe na kuadabishwa. Pili, tatizo la Ukimwi lina vyanzo vyake kama vile umaskini.

Tunashughulika vipi na kuutokomeza umaskiniwa mtanzania aishie kwenye (absolutely poverty) kumjengea mazimgira ya kuwa na uwezo wa kupambana na Ukimwi? Hata kama Ukimwi hauchagui maskini na tajiri lakini kwa “makapuku” na “malofa” wako kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa Ukimwi hususani watoto wa kike.

Tunaweza kufanikisha Tanzania isiyo na Ukimwi kama tutaongeza juhudi za kupambana na Ukimwi naam zitakuja nyakati tutaona kuwa Ukimwi umebaki katika historia. Swali nini kifanyike sasa? Tufanye kazi kwa bidii na uaminifu, tuache matendo ya hovyo, tumlilie Mungu na Mungu wetu yupo, anasikia na atafanya, naam Tanzania itabaki salama bila Ukimwi.

Wilaya za Mbeya, Rungwe na Ilala ni mfano bora kuwa Ukimwi kwamba unaenda kuwa historia nchini kutokana na kupungua kwa maambukizi ya Ukimwi kutoka asilimia saba hadi asilimia nne tu katika kipindi kifupi kilichopita.

nkwabicharles@yahoo.co.uk Simu 0754 555680

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home