Monday, December 17, 2007

Watanzania wale majani?

Na: Charles Nkwabi – Tabora

Nani mwenye jeuri ya kuishi bila kula chakula dunia hii? Hakuna maisha pasipo chakula. Tunaishi kwa sababu tunakula chakula. Tutaniane kwenye masuala mengine Si ubishi hata matahira huwa wanaokota vyakula kwenye majalala, ingawa huwa haijulikani mara moja nani huwatuma wehu na matahira waende kwenye majalala kuokota chakula wale ili waishi! Tunakula ili tuishi na si kuishi ili tule.

Cha ajabu na kushangaza hapa Tanzania suala la chakula hakuna anayelijali. Ni ”longolongo na kejeli. Ni wimbo tu eti ”uti wa mgongo wa Tanzania ni kilimo”. Ni ubabaishaji tu na porojo nyingi, ni maneno matupu yanayovuma kama debe tupu linapopigwa na upepo.

Siku ya chakula duniani, kitaifa iliadhimishwa Mwanza, wananchi waliadhimisha siku hiyo bila chakula, walishinda na njaa huku wakiburudishwa kwa ngoma!

Athari za kukosa chakula zinalidhalilisha taifa letu mpaka wenzetu nchi zilizoendelea ”wanatushangaa sana” na kutuhurumia, hivi kichwani sisi hamnazo? Fyuzi za kichwani zimefyatuka? zimechomolewa? Tuna ardhi kubwa yenye rutuba, chochote ukipandacho kinaota na kukua, tatizo? Viongozi wetu ni wazembe? Wameridhika na maisha ya wale wanaowaongoza? Maswali ni mengi kama kilivyo kichwa cha makala hii..

Wabunge wetu wawabane mawaziri, naam jamii nzima ikemee mtindo uliozuka wa kuwakumbatia wageni wakipata mikopo kwenye mabenki ya ”kibongo” halafu wabongo wanawekewa ”mizengwe” kukopeshwa! Wenye nchi ni kama takataka, wageni ndio ”watu”

Inatia simanzi kwani benki inayomilikiwa na serikali benki ya rasilimali (TIB) haiwakopeshi wakulima! Mabunge wetu juzijuzi wamekuja juu wakiwalalamikia mawaziri bungeni!

Huwezi kuwa taifa kubwa, ukajenga uchumi wako vizuri, ukajipanua teknolojia na kuwa na maendeleo kama unakidharau kilimo. Mbona kila wakati mtu akipatwa njaa huwa analalamika na kutafuta hotel iko wapi ili ale ashibe na akishashiba anakuwa na jeuri ya shibe?

Jamaa mmoja mzungu alikataa kuongea na mimi nilipomkuta akiwa na njaa kali wakati wa mchana akasema ”sasa nina njaa kali siwezi kukusikiliza, njoo baadae nitakuwa nimekula! We!hakuna mwenye jeuri kwenye njaa, awe mzungu awe nani wote ni foleni mbele ya chakula!

Akiwa kama rais wa nchi Mwalimu Julias Nyerere alikuwa ni mfano wa kuigwa, ndio rais wa nchi alikuwa mkulima hodari, ingawa hakuwa mfanyabiashara alikuwa na chakula cha kutosha. Mwalimu alijali sana kilimo watu wake wawe na chakula cha kutosha.

Mwalimu aliwalazimisha watu walime mashamba ya pamoja, kwanza mwenyewe akiwa mfano kijijini kwake Butiama ana mashamba kibao. Haombi mtu chakula hata leo familia yake ina utajiri wa chakula!

Leo hii sisi huwa tunaona fahari sana tunapopungukiwa na chakula na kuanza kutoa visingizio mbalimbali kwamba mvua hazinyeshi kwa utaratibu unaotakiwa! Tunaona fahari kuomba chakula kwenye mataifa mengine, wakati mwingine mvua ikichelewa tunasema ”tuna janga la ukame! Hivi hatuna wataalamu nchi hii? Tunapotegemea mvua tu, tuna mkataba na Mungu kwamba lazima kila mwaka mvuaitanyesha?

Mosi, wataalamu wetu wa kilimo utadhani wanafanya maigizo kwenye kilimo. Mashamba yako vijijini wao wanaishi mijini na hawatoi elimu ya kilimo kwa wananchi vijijini. Wananchi vijijini hawapati elimu ya kilimo, tembea vijijini ujionee..

Pili wataalamu wetu wa kilimo waliosomeshwa na serikali wengi wao wanafanya kazi kwenye sekat binafsi, wameajiriwa na makampuni kama ATTT. Serikali imejiingiza mkenge yenyewe. Naambiwa masilahi serikalini hayatoshi!

Tatu wataalamu wetu wa kilimo waliobakia yumkini hawajawezeshwa (empowered) na serkali kwamba haina bajeti ya uchimbaji wa mabwawa ama wao wataalamu hawa hawana fikra pevu za kuweza kubuni njia rahisi ya kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji ambayo yanaweza kutumika wakati mvua hazinyeshi. Wananchi wakishirikishwa wanaweza. Tunapopata tatizo la ukame mawaziri wetu ndio wanachakarika kutafuta suluhisho! Na visingizio gunia!

Wakati mwingine wananchi wanaishia kuhubiriwa kuwa kuna mvua ya kutengeneza itakuja kutoka nchi fulani.. Hawana mpango, wala hakuna mikakati ya kuwa na bajeti angalau kila tarafa wawe na bwawa lao moja la kuendeshea kilimo cha umwagiliaji..

Mbolea ndio suala gumu kupindukia. Imefikia wakati wabunge wetu kulipigia kelele suala hili bungeni ili serikali ipunguze bei ya mbolea ili wakulima waweze kumudu kununua lakini wapi, hasikilizwi mtu! Mbunge wa Nzega CCM Lucas Seleli ni mfano wa kuigwa, alilipigia kelele sana suala la bei ya mbolea serikali iingilie kati kupunguza ushuru wa mbolea na kuwabana ”maghabachori” yanayowanyonya wananchi, nani anajali kila mtu ”anajiju” kivyake, hii ndio ”bongo dar es salaam”!

Maskini wa Mungu wanavijiji wanalima sana kwa jembe la mkono mpaka wanapinda migongo yao, mtu analima heka tano anavuna magunia matatu ya mahindi huku ana familia kubwa anakimaliza chakula kwa muda wa miezi sita tu baadae ankuwa ombaomba!

Pembejeo ziko bei juu sana kiasi ambacho hakuna mikakati ya kuwawezesha wananchi kujipatia pembejeo hizo kwa bei nzuri. Kama ipo mikakati hiyo basi iko kwenye makaratasi na viongozi wahusika wa kilimo wamelewa madaraka, pengine wanangoja watu waanze kufa kwa njaa ndio washtuke, si ndivyo ”wabongo” tulivyo?

Maji wanayokunywa wanajiji ni ya kwenye malambo utadhani nao ni sawa na mbuzi au ngombe hata wanyama wanahitaji kunywa maji safi na salama! Hivi haiwezekani kila kijiji kikawa na visima hata vitatu ama vinne vinavyotoa maji safi na salama? Mbona ugonjwa wa bonde la ufa ulifanyiwa mikakati ya kudhibitiwa sana kuliko suala la chakula.

Hivi hatujui kwamba mtu akinywa maji yasiyo salama anaweza kuugua na kama hapati dawa atakufa tu kama mgonjwa wa bonde la ufa? Hivi hatujui vyanzo vya umaskini uliopita mipaka uliopo kijijini? Kijijini wanahangaikia mlo wa siku moja kwa hiyo hawana muda mwingine wa kujitafutia vipato!

Ni akina nani huko vijijini wanaofahamu juu ya mkakati wa kupunguza umaskini na kuongeza vipato – MKUKUTA? Tena ni wangapi wenye taarifa juu ya mkakati wa kupunguza umaskini binafsi –MKUKUBI?

Kwa mfano kama mama wa nyumbani anayafuata maji umbali mrefu mpaka masaa saba ndio anarudi nyumbani, saa ngapi atampikia mumewe chakula ili waishi? Shime usanii kwenye maswala ya utawala uwe mi marufuku. ”Ushikaji – shikaji” na ujanja ujanja wa kukwepa majukumu ya kuwahudumia wananchi upigwe vita kama ugonjwa wa bonde le ufa! Kama mtu ameshindwa kazi ya kuwatumikia wananchi hata kama amesoma aondoke haraka kabla hajaondolewa, asiwafanye watanzania wakala majani, watanzania sio ngo’mbe, ni binadamu.

E- mail:
nkwabicharle@yahoo.co.uk Simu: 0754 555680

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home