Monday, December 17, 2007

Nani anaizimisha kasi mpya?

Na: Charles Nkwabi – Tabora

Ahadi ni deni. Rais Kikwete kwenye hotuba yake ya kwanza bungeni aliahidi kushughulikia suala la kuunda kamati ya kuchunguza mikataba ya madini. Watanzania walisubiri kwa hamu kubwa utekelezaji wake wasione kitu hadi wakaanza kushtuka huku baadhi yao wakijiuliza, “hivi kasi mpya nani anaizimisha?

Ukisikia kasi mpya ujue ni awamu ya nne ambayo inajulikana kwa jina la JK4. Rais wetu ndugu Jakaya Mrisho Kikwete ndiye aliyekuja na kauli hii ya aina yake ya kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya na hata bunge letu likaitwa “speed and standard parliament”.

Kikwete ni kiongozi mwenye mvuto kwa watu. Ameanza kutengeneza historia ya aina yake na bado tutaona na kusikia mengi akiyafanya. Inawezekana Kikwete akawa ni kiongozi wa kuzaliwa au wa kuendelezwa. Ninachojua viongozi huzaliwa wakiwa na kipaji cha kuongoza huku baadhi ya watu huendelezwa wakawa viongozi wazuri sana .

Akili kubwa, akili pevu huongelea mada au mambo makubwa yanayogusa mustakabali wa maisha ya watu na jamii kwa ujumla. Ni kwa msingi huu nachelea kuandika makala hii juu ya mambo mazito yanayogusa kila mtanzania mpenda maenedeleo.

Safu hii imekuwa kimya kwa muda mrefu kwani haikuwepo nchini lakini kupitia mitandao ilikuwa inafuatilia kwa karibu sana yanayojili huko “bongo dar es salaama”. Safu hii ilikuwa ikipata matukio yote makubwa kama vile kifo cha Amina Chifupa na mengineyo mengi.

Alipoingia madarakani JK alikuwa “amepanda sana chati” hasa kupitia hotuba zake za kusisimua na kuleta matumaini hasa kwa walalahoi wa nchi hii. Kikwete alitangaza mambo ya kushughulikia kama Rais wa nchi.

Mosi, Suala la kupitia upya mikataba ya madini ni suala nyeti saana. Mbunge mmoja alipohoji suala la mkataba wa madini kusainiwa London na kuomba kwamba tume iundwe kuchunguza suala hilo , mbunge huyo (Zitto Kabwe) alihukumiwa na bunge huku “pilato” (Spika wa bunge) akibariki kutimuliwa kwa Zitto Kabwe.

“Mafisadi, watafuna nchi hawa, mjadala wa madini waibua jipya CCM, Kikwete azidiwa kete, Mkapa akana tuhuma za ufisadi, watafuna nchi hawa”, na majina ya mafisadi yavuja” ni baadhi ya vichwa vya habari kwenye magazeti vilivyokuwa vinawasha masikio na macho ya watanzania.

Naam hali ya hewa ikachafuka kwa viongozi wetu. Kikwete akawa kwenye kipindi kigumu. Kwenye mkutano mkuu wa nane wa uchaguzi mkuu wa CCM pale mjini Dodoma , alisema “ kama viongozi tunapitia vipindi vigumu. Ukiwa kiongozi, kipindi kigumu ni kipindi cha kutulia, ukihamanika na ukababaika utatoa maamuzi ya ajabu sana . Naam ni dhahiri shahir Kikwete “ametikiswa” na sauti ya umma, wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali na wadau, wapenda maendeleo wakihoji juu ya mafisadi na mikataba ya madini yenye utata.

Mtikisiko kwa rais Kiwete ulianzia bungeni wakati Zitto Kabwe “alipotimuliwa” bungeni, naam Zitto akawa amezua zito nchini. Vyama vya upinzani Chadema, TLP, CAF vikaanza kupiga kelele hatimae nchi wahisani nao wakaanza kushtuka! Wananchi nao wakashtuka!

Katika mkutano mkuu wa nane wa CCM pale Dodoma uliomalizika siku za karibuni, Kikwete alibainisha kuwa rushwa inafanyika ndani ya wanaCCM. “Aliyetoa dau kubwa la nauli na posho kwa wajumbe ndiye anayepita kuwa kiongozi hata kama hana maadili ya uongozi” alisema Kikwete na kuongeza “Rushwa inaleta tabaka kati la kundi la wenye nacho kuwa miungu watu dhidi ya makabwela”

Naye Katibu mkuu wa CCM Yusufu Makamba akitoa hotuba yake kwenye mkutano Mkuu wa CCM alisema “suala la rushwa wote tunahusika, tusilaumiane”. Hii ina maana viongozi wetu mpaka chama tawala CCM wanahusika kugawa na kupokea rushwa maana ndio mtindo sasa!

Baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa CCM pale Dodoma, news zinasema kuwa Kikwete alipokelewa “bongo” kwa shangwe na wananchi kutokana na hotuba yake aliyoitoa pale Dodoma . Kubwa zaidi ambalo Kikwete ameonyesha kweli ni mchapakazi ni suala la kuunda tume ya kuchunguza mikataba ya madini inayojumuisha wajumbe kutoka kambi ya upinzani akiwemo Zitto Kabwe.

Changamoto iliyopo ni juu ya hiyo tume iliyoundwa na Kikwete: Ikipigwa “upofu” na “kuleweshwa” na mifumo ya kujuana na kulindana, hali itakuwaje?

Pili, Kikwete alilivalia njuga suala la nyumba za taifa zilizokuwa zimepigwa bei ya kutupa, “bei poa” enzi za rais mstaafu Benjamin Mkapa, watu waliuziana nyumba za serikali kwa kujuana na wakapeana naam ndivyo ilivyo kwa watanzania kila kitu ni mjuano, kama hujulikani “utajiju”.

Suala la nyumba baada ya kipindi takribani miaka miwili sasa tangu JK aingie madarakani, suala hilo limeminywa, na kufichwa, halifuatiliwi na rais wetu…swali, nani anaizimisha kasi mpya?

Ukiangalia nyumba zaTanzania yetu, maghabachori, yamezikalia nyumba zote za maana
katikati ya miji yetu, nenda Mwanza, Bukoba, Shinyanga, Tabora mpaka “bongo” huna haja ya kuambiwa tazama. Wazalendo wako nje pembeni mwa miji huku baadhi yao wanaishi kwenye mbavu za mbwa, hii ndio Tanzania .

Jiulizeni kuhusu India , hivi kuna wabongo wanaohodhi nyumba kule India huku wenyeji wakihangaikia makazi? Thubutu! Wamelogwa! Bahati nzuri Tanzania tunapenda saana sifa ya ukarimu mpaka nyumba zinapigwa minada kwa bei ya nyonyofo kisha watumishi wa serikali wanahaha kupanga nyumba uswahilini! Mfumo uliopo wa mjuano mpaka serikali inahaha huku baadhi ya watumishi wake wakiishi hotelini ni kitendo cha aibu kwa taifa. Taifa letu linaghilibiwa na wageni.

Kuna mikataba feki naya kishenzi kama vile ya Richmond inaonyesha wazi kuwa maisha ya watanzania si lolote si chochote na maisha yamewekwa rehani huku wabongo wakiishi gizani bila umeme! Je kasi mpya itayavalia njuga masuala haya yote na kuzirudishwa nyumba za serikali au kasi hii ni moto wa mabua? Kasi mpya itatengeneza historia inayotarajiwa? Yetu macho na masikio mpka mwaka 2010.

E – mail:
nkwabicharles@yahoo.co.uk simu: 0754555680

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home