Walimu wamtesa JK
Tabora
RAIS Jakaya Kikwete, amesema madai yasiyokwisha ya malipo mbalimbali ya walimu nchini, yanathibitisha kuwa baadhi ya viongozi, ama wana ukosefu wa kiwango kikubwa cha ufanisi, ama ni wadanganyifu.
Rais Kikwete, alisema hayo juzi wilayani hapa baada ya kupokea taarifa ya utendaji ya Wilaya ya Tabora katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku nane mkoani hapa.
“Ama sisi viongozi ni wakosefu wakubwa wa ufanisi, ama na sisi tumekuwa wadanganyifu. Huwezi mwezi huu ukalipa sh bilioni saba, na miezi mitatu baadaye ukaletewa madai mengine ya sh bilioni 12. Haiwezekani, madeni haya yakawa hayaishi. Hatuwezi kuendelea ‘to run in circles’ kama wanavyosema Waingereza.
“Jibu la udanganyifu ni kupelekwa kortini na kufungwa. Jibu la kukosa ufanisi kwa mtumishi wa umma ni kuondolewa katika nafasi yake na akapatikana mtu mwingine wa kufanya kazi,” alisema Rais Kikwete.
Rais aliambiwa kuwa walimu katika wilaya hiyo walikuwa bado wanaidai serikali, hata baada ya baadhi ya madeni yao kuwa yamelipwa.
Ilielezwa kuwa walimu katika wilaya hiyo wanaidai serikali sh milioni 93, ikiwa ni posho ya likizo na kujikimu, hata baada ya kuwa wamelipwa baadhi ya madai yao Machi, mwaka huu.
“Kama nilivyosema juzi Sikonge, nataka hili limalizike kwa kufanya uhakiki wa shule kwa shule, mwalimu kwa mwalimu, kichwa kwa kichwa, ili tujue nani hasa anadai nini. Baada ya kupata uhakika huo, wale wanaodai tutawalipa, ili tuondokane na madai haya yasiyoisha.
“Lazima tukate mzizi wa fitina. Nataka madeni haya yalipwe baada ya kuwa yamehakikiwa. Lazima tumalize misuguano hii. Mwezi Machi tumelipa sh bilioni saba, miezi mitatu baadaye tunaletewa madai mengine ya sh bilioni 12. Sasa nataka hili limalizike kwa namna ya kudumu,” alisema rais.
Kuhusu malalamiko ya uongozi wa wilaya hiyo kuwa hauna nafasi ya kutosha kujenga hospitali ya wilaya, rais aliwataka viongozi hao kuacha kulalamika.
“Nyie viongozi acheni kulalamika na kunung’unika. Fanyeni uamuzi. Ama jengeni hospitali ya wilaya katika eneo la wilaya jirani ya Uyui, ama jengeni mjini kwa kupandisha ghorofa kama hamna ardhi ya kutosha,” alisema Rais Kikwete.
Rais alikuwa ameambiwa kuwa uongozi wa wilaya hiyo unataka kujenga hospitali ya wilaya, lakini hauna ardhi ya kutosha kuweza kujenga hospitali yenye hadhi hiyo.
Wakati huo huo, Rais Kikwete, ameonya tabia ya baadhi ya waajiri nchini kuwalipa mishahara kidogo wafanyakazi wao, kuwa itazua migogoro na wafanyakazi wao.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa waajiri wanawakabidhi wafanyakazi mashine za mamilioni ya fedha, wazilinde na kuzitumia, lakini wakati huo wanawalipa mishahara kidogo.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo jana, alipokuwa akikagua kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha New Tabora Textile Mills cha mjini Tabora na kuzungumza na wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho.
“Ni jambo gumu kidogo kueleweka. Mnawakabidhi wafanyakazi wenu mashine na mitambo ya mamilioni ya fedha, lakini bado mnawalipa mishahara kiduchu.
“Msibane masilahi ya wafanyakazi. Mnaweza kuwalipa mishahara kidogo kwa muda, lakini hatimaye hili litawaingiza katika migogoro na wafanyakazi wenu,” alisema.
Hata hivyo, rais ameusifia uongozi wa kiwanda hicho kwa kuonyesha mfano wa nini kinatakiwa kufanywa na viwanda vya nguo nchini.
“Nashukuru na kuwapongeza sana kwa sababu nyie mmeonyesha mfano. Tusiishie kwenye kuchambua pamba tu, tusiishie kwenye ginnery tu. Hatua inayofuata sasa ni kutengeneza nyuzi na hatimaye kutengeneza nguo hapa hapa nchini,” alisema.
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home